MWALIM U ACHAPWA MAKOFI MBELE YA WANAFUNZI


MKUU wa Shule ya Sekondari Kabwe iliyopo mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Nkasi Mkoa wa Rukwa, Jackson Mussa anatuhumiwa kumshambulia mwalimu mwenzake, Emmanuel Mbemba kwa kuchapa makofi huku wanafunzi wao wakishuhudia tukio hilo.
Mbemba anafundisha Kidato cha Tatu Somo la Jiografia. Ofisa Elimu Kata ya Kabwe, Geoffrey Mtafya amethibitisha kutokea kwa tukio hilo. Alieleza kuwa lilitokea juzi Alhamisi asubuhi shuleni hapo na kusababisha taharuki kubwa kwa wanafunzi na jumuiya ya shule hiyo.
Akisimulia mkasa huo, alisema asubuhi hiyo ya tukio, Mwalimu Mbemba alienda ofisini kwa Mussa na kumuomba ruhusa ili aende ziara ya mafunzo kwa kutembelea fukwe za Ziwa Tanganyika.
"Mwalimu Mkuu (Mussa) alimtaka mwalimu huyo huyo andike barua ya kiofisi ambapo alifanya hivyo... Mussa alimweleza mwalimu huyo kuwa baada ya muda si mrefu atampatia majibu kwa maandishi,” alieleza.
Aliongeza kuwa Mwalimu Mbemba alimfuata mkuu wa shule, ambaye alimueleza kuwa aendelee kusubiri, kwani alikuwa hajaiandika barua ya kumpatia ruhusa, kwa kuwa alikuwa na majukumu mengine.
"Mwalimu Mbemba alimfuata mkuu wa shule mara ya tatu na alimweleza kuwa anachelewa kwenda kwenye ziara ya mafunzo na wanafunzi wa Kidato cha Tatu ...ndipo mkuu wa shule alipotaharuki na kumkaba koo Mwalimu Mbemba mbele ya wanafunzi na akaanza kuzaba vibao mfululizo,” alidai ofisa elimu kata.
Taarifa kutoka shuleni hapo zilidai kuwa wanafunzi na jumuiya ya shule hiyo, walishuhudia tukio hilo huku baadhi yao wakishangilia na kuzomea.
Mtafya alisema Mbemba alitoa taarifa kwa Kiongozi wa Chama cha Walimu (CWT) mahali pa kazi, Elia Elia aliyemtaarifu Ofisa Mtendaji Kata ya Kabwe, Geoffrey Kuzumbi ambaye aliitisha kikao cha dharura shuleni hapo.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho, zinaeleza kuwa Mkuu wa Shule, Mussa alikana kumpiga makofi mwalimu Mbemba akisisitiza kuwa alimkaba koo. Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Nkasi, Abel Ntupwa alikiri kutokea kwa tukio hilo ambalo alililaani. Alisisitiza kuwa ni utovu wa nidhamu na kwamba atalitolea maamuzi Jumatatu baada ya kupatiwa ripoti kamili.
Previous
Next Post »