Ripoti: Wengi pwani ya Tanzania kuwa hatarini

Tanzania ni miongoni mwa nchi 25 duniani ambazo zitakuwa na watu wengi maeneo ya pwani walio katika hatari ya kuathiriwa na mafuriko kutokana na mabadiliko ya tabia nchi kufikia mwaka 2060.
Shirika la Christian Aid la Uingereza, kwenye ripoti yake, linasema Tanzania itakuwa na watu 14 milioni katika pwani yake ambao watakuwa katika hatari ya kuathiriwa na mafuriko.
Kufikia mwaka 2000 idadi hiyo ilikuwa 600,000 pekee lakini kufikia mwaka 2030 watakuwa wamefikia 2.8 milioni.
Afrika Mashariki, taifa jingine ambalo limo kwenye orodha ya nchi 25 ni Somalia, ambayo itakuwa na watu 9.8 milioni watakaokuwa hatarini 2060.
Nchini Msumbiji, ambapo kulikuwa na watu 2.3 milioni waliokuwa hatarini 2000, kufikia mwaka 2060 kutakuwa na watu 7.5 milioni watakaokuwa hatarini.
China ndiyo inayoongoza duniani ambapo watu 244.8 milioni watakuwa hatarini kufikia 2060 ikifuatwa na India na watu 216.4 milioni.
Ripoti hiyo iliyopewa jina Act Now Pay Later, (Chukua hatua sasa, malipo baadaye), inasema kufikia mwaka 2060 watu zaidi ya bilioni moja duniani watakuwa hatarini ya kuathirika na mafuriko kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
Nchi zinazotoa gesi zinazochangia ongezeko la joto duniani kwa wingi – China, India na Marekani, ndizo zinazokabiliwa na hatari zaidi ya maafa.
Miji miwili ya India, Kolkata na Mumbai, ndiyo inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu walio hatarini. Inafuatwa na mji wa Dhaka, Bangladesh na mji wa Guangzhou nchini Uchina.
Mji wa Alexandria nchini Misri ndiyo unaoongoza Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya watu walio hatarini. Unafuatwa na mji wa Lagos, Nigeria na Abidjan nchini Ivory Coast.
Ripoti hiyo inayahimiza mataifa kuchukua hatua haraka kupunguza athari za ongezeko la joto duniani.
TaifaMamilioni ya watu watakaokuwa hatarini 2016
1. China244.8
2. India216.4
3. Bangladesh109.5
4. Indonesia93.7
5. Vietnam80.4
6. Misri63.5
7. Nigeria57.7
8. Marekani43.9
9. Thailand36.8
10. Ufilipino34.9
11. Japan32.7
12. Pakistan30.1
13. Myanmar22.8
14. Senegal19.2
15. Brazil18.7
16. Iraq18.1
17. Benin15.0
18. Tanzania14.0
19. Uholanzi11.8
20. Malaysia11.3
21. Somalia9.8
22. Uingereza8.8
23. Côte d’Ivoire7.6
24. Argentina7.6
25. Msumbiji7.5
Previous
Next Post »