Usafiri wa unga EAC wajipanga safari za ulaya,USA


KAMPUNI za ndege za Air Tanzania Limited (ATCL), Kenya Airways (KQ) na Rwandair zinatekeleza mikakati ya kujiimarisha ikiwa ni pamoja na kuanzisha safari za Ulaya, Marekani na Asia, kununua ndege mpya, na kusaini mikataba kukuza biashara.
Julai mwaka huu, ATCL inatarajia kupokea ndege kubwa za abiria, ikiwemo aina ya Boeing 787 yenye uwezo wa kubeba abiria 262. Januari 17 mwaka huu, kampuni hiyo ilitangaza nafasi za kazi 88 za wahudumu kwenye ndege.
Hatua hizo zimeelezwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa kuwa ni mchakato wa kuiboresha ATCL kwa lengo la kukuza biashara ndani na nje ya Tanzania kuliwezesha kuongeza mapato na kukuza uchumi wa taifa.
Profesa Mbarawa alisema, ili kuiboresha ATCL, Serikali imeshanunua ndege mpya mbili aina ya Bombadier Dash 8-Q 400 zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja. Ndege hizo zimetengenezwa Canada, na ziliwasili nchini mwaka jana
“Baada ya ununuzi wa ndege hizo, hatua inayofuata ni ununuzi wa ndege nyingine tatu zikiwemo mbili aina ya CS 300 zenye uwezo wa kubeba abiria kuanzia 150-160 pamoja na ndege moja kubwa aina ya Boeing 787 itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 262, zinazotarajiwa kuwasili kwa pamoja ifikapo Julai mwaka huu,” alisema.
Waziri Mbarawa alisema, ununuzi huo utaiwezesha ATCL kufikisha ndege mpya tano zitakazosaidia kuongeza safari zake kwa kuhudumia masoko yake ya ndani na ya nchi jirani kama vile Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Malawi, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Kwa mujibu wa tovuti ya kampuni hiyo, ATCL inaamini kwamba, kwa kuongeza idadi ya ndege itakuwa mshindani wa uhakika kwenye soko. Programu ya kujitanua ya kampuni hiyo ina lengo la kufanya biashara Afrika, Ulaya, Asia na Marekani.
Machi mwaka jana, ATCL na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) walisaini mkataba wa makubaliano (MoU) ambao pamoja na mambo mengine utaliwezesha shirika hilo kujitangaza kupitia kazi za bodi hiyo na pia wafanyakazi wake wakiwemo marubani na wahudumu kwenye ndege kufundishwa namna ya kutangaza vivutio vya utalii.
Kwa kuzingatia mkataba huo, ATCL pia itapata fursa ya kutangaza huduma zake kwenye maonesho ya utalii yanayoandaliwa au kuhudhuriwa na TTB. Mikakati ya Rwandair Shirika la Ndege Rwanda, Rwandair limetangaza zabuni kupata kampuni itakayouza tiketi zake kwenye soko la Israel kupitia utaratibu wa Wakala wa Mauzo wa Ujumla (GSA).
Kwa mujibu wa tangazo kwenye tovuti ya kampuni hiyo ya Serikali, Rwandair inakaribisha waombaji wenye sifa kuomba kuwa GSA wa Rwandair nchini Israel. GSA ni mwakilishi wa mauzo wa shirika la ndege kwenye eneo au nchi fulani ambako kampuni husika haina ndege inayokwenda huko ila inaweza kupata wateja.
Tangu Februari pili mwaka huu, nyaraka kamili za zabuni kwa lugha ya Kingereza zinapatikana ofisi kuu za Rwandair kwenye Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kigali. “Zabuni lazima ziwe zimewasilishwa kabla ya saa 10.30 asubuhi (saa za Rwanda) Machi 03, 2018” inasomeka sehemu ya tangazo la Rwandair kukaribisha waombaji.
Rwandair inafika kwenye zaidi ya miji 20 ya mashariki, magharibi, kusini mwa Afrika, Afrika ya kati, mashariki ya kati, Asia na Ulaya. Agosti mwaka jana, kampuni hiyo ilizindua kituo cha biashara Benin ili kihudumie Afrika ya kati na magharibi.
Waziri wa Nchi anayeshughulikia Usafirishaji Rwanda, Jean de Dieu Uwihanganye amesema, Mei mwaka huu, Shirika la Ndege la Rwandair linatarajia kuanza safari za Guangzhou, China.
Amesema, shirika hilo pia linapanga kuanza safari za moja kwa moja kwenda New York, Marekani. Alisema, safari kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Guangzhou Baiyun, kwenye jimbo la Guangdong zitapitia ruti ya Mumbai, India, na kwamba, wanatafuta uwezekano wa kuwa na safari za moja kwa moja baadaye.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Sekta Binafsi (PSF) nchini humo, Benjamin Gasamagera, amesema, safari za China zitakuza biashara si tu kwa Rwanda ila pia kwa ukanda wa Afrika.
Mikakati ya Kenya Airways Kuanzia Oktoba 28 mwaka huu, Shirika la Ndege la Kenya (KQ) litaanza safari za moja kwa moja kutoka uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) jijini Nairobi kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa John F. Kennedy (JFK), New York, Marekani.
KQ inaendelea kuuza tiketi za safari hizo za kila siku. “Kuanza kwa safari za moja kwa moja kati ya Kenya na Marekani itakuwa hatua muhimu kwa biashara na kwa nchi,” amesema Mwenyekiti wa KQ, Michael Joseph.
KQ inatarajia kuwa wateja wengi kwa safari hizo za kila siku watakuwa watalii na wafanyabiashara. Ndege za KQ zinatarajiwa kusafiri kwa saa 15 kutoka JKIA kwenda JFK.
Previous
Next Post »