Yanga yaipania TP Mazembe


WAWAKILISHI pekee wa Tanzania katika michuano ya kimataifa, Yanga baada ya kupoteza mchezo wake wa ugenini dhidi ya Mo Bejaia ya Algeria, wamepania kumaliza hasira zote kwa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Yanga itacheza na mabingwa hao wa zamani wa Ligi ya Mabingwa wa Afrika Juni 28 kwenye Uwanja wa Taifa na wanatarajia kurejea nchini siku mbili kabla ya mchezo huo. Katika mchezo huo uliochezwa juzi usiku kwenye Uwanja wa Unite Maghrebine mjini Bejaia, Algeria, Yanga ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga kushika nafasi ya tatu kwenye kundi A huku TP Mazembe wakiongoza baada ya kushinda 3-1 dhidi ya Medeama ya Ghana, nafasi ya pili ikishikiliwa na wapinzani wa Yanga, Mo Bejaia na wa mwisho ni Medeama.
Akizungumza na gazeti hili jana Kocha Msaidizi wa Yanga Juma Mwambusi alisema walijipanga kufanya vizuri na kwamba licha ya kuonesha uwezo hasa kipindi cha pili, walifungwa kutokana na makosa yao.
Alisema wachezaji wa Mo Bejaia walitumia vizuri makosa ya Yanga na kupata bao hilo moja, lakini wachezaji wa Yanga walishindwa kufunga licha ya kupata nafasi nyingi langoni mwa wapinzani wao.
“Tulifanya makosa madogo ambayo yalitugharimu, lakini ndio sehemu ya mchezo na sasa tunaangalia namna ya kujipanga upya kwa mchezo wetu ujao dhidi ya TP Mazembe ili kufanya vizuri katika mchezo wa nyumbani,”alisema.
Mwambusi alizungumzia pia kuhusu wachezaji wake kukosa nidhamu na kupewa kadi nyingi za njano, alisema suala hilo wameliona na watalifanyia kazi katika kambi ya Uturuki ili kuwaelimisha wachezaji hao kuwa na nidhamu mchezoni hasa ugenini.
Katika mchezo huo baadhi ya wachezaji wa Yanga walioneshwa kadi za njano, ambao ni Donald Ngoma, Simon Msuva na Amis Tambwe huku Mwinyi Haji akitolewa kwa kadi nyekundu dakika za nyongeza za mchezo huo.
Kocha huyo wa zamani wa Mbeya City alisema watarekebisha mapungufu yao ili kumaliza hasira zao katika mchezo ujao wa TP Mazembe utakaochezwa Jumanne ya wiki ijayo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kikosi cha Yanga kilitarajiwa kuondoka Algeria jana jioni na kurudi Uturuki kuendelea na kambi ya wiki moja ya maandalizi ya mchezo huo kabla ya kuondoka Juni 26 kurudi Dar es Salaam kuikabili TP Mazembe.
Wakati huo huo, Meneja wa Yanga Hafidh Salehe alisema wanahitaji kuwaelimisha wachezaji namna ya kuwa makini na waamuzi hasa katika mechi za ugenini ili kukwepa kulimwa kadi bila mpangilio.
Alisema waamuzi waliochezesha mchezo dhidi ya Mo Bejaia walikuwa wanatoa kadi hata pasipostahili. Mechi hiyo ilichezeshwa na waamuzi kutoka Morocco, Bouchaib El Ahrach aliyekuwa kati, akisaidiwa na washika vibendera, Redouane Achik na Youssef Mabrouk.
Previous
Next Post »