Mwili wa wakili aliyetoweka Kenya wapatikana

Mili miwili imepatikana nchini Kenya wakati wa usakaji wa wakili mmoja aliyetoweka wiki moja iliopita akiwa na mteja wake na dereva wa taxi.
Awali afisa mkuu wa kitengo cha jinai nchini Kenya Ndegwa Muhoro alinukuliwa na gazeti la Daily Nation akisema kuwa juhudu za kuutafuta mwili wa tatu unaodaiwa kuwa wa mteja wa Bw Kimani ,Josphat Mwenda zinaendelea.
Afisa mkuu wa polisi nchini humo tayari ameagiza kukamatwa kwa maafisa watatu wa polisi wanaoshukiwa kuhusika na utekaji nyara wa wakili Willie Kimani.
Bw Kimani alikuwa akimwakilisha mteja wake aliyekuwa akiwasilisha malalamishi dhidi ya polisi.
Chama cha wanasheria nchini kinaamini kwamba alitekwa nyara baada ya kuondoka mahakamani katika mji mkuu Nairobi.
Duru za polisi zimeambia BBC kwamba mili miwili ilipatikana kandokando ya mto yapata kilomita 70 kaskazini mashariki mwa Nairobi.
Usakaji unaendelea katika eneo hilo ili kuupata mwili mwengine wa tatu kulingana na gazeti la Kenya,The Standard.
Bw Kimani alikuwa akilifanyia kazi shirika moja la hisani kuhusu sheria nchini Marekani, International Justice Mission ambalo huzingatia visa vya maafisa wa polisi wanaotumia vibaya mamlaka yao.
Previous
Next Post »