NEC yafikiria mfumo wa kuwezesha watanzania kupiga kura popote walipo


TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema inaangalia uwezekano wa Watanzania kupiga kura wawapo sehemu yeyote nchini badala ya kulazimika kuwa kwenye vituo walivyojiandikisha.
Alisema wakati sasa sheria inaangalia sehemu mtu alipojiandikisha, wameona changamoto hiyo kutokana na upungufu kwenye uchaguzi uliopita, hivyo wanatafuta ufumbuzi mwenye uchaguzi ujao.
Akizungumza katika Maonesho ya 40 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere, barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva alisema suala hilo wamelipata na wataangalia ni vipi sheria itaruhusu katika uchaguzi ujao.
Alisema baada ya kukamilisha uchaguzi uliopita na kuwasilisha ripoti kwa Rais, Dk John Magufuli, wanakuwa wamekamilisha mzunguko wa uchaguzi uliopita na wanajiandaa na uchaguzi unaokuja.
Alisema kuelekea uchaguzi ujao, wanaanza uandikishaji na wanakusudia utakuwa endelevu badala ya kusubiri kuanza kazi hiyo katika na uchaguzi mwingine.
“Tukifika uchaguzi ujao kuwa tumekamilisha mambo mengi bila kufanyika mwishoni kama uchaguzi uliopita,” alisema.
Akizungumzia tume huru ya uchaguzi, alisema wengi wanadhani kuwa na jina inatosha wakati ukweli ni utendaji kazi kusimamia na kufanya kazi bila kuingiliwa.
“Naweza kujisifia kwa tume niliyonayo ni huru, kwani tangu chaguzi zote hakuna kiongozi aliyeingilia na kutaka kupendelea fulani hivyo ni huru kiutendaji,” alisema.
Previous
Next Post »