WAZIRI WA VIWANDA AFANYA ZIARA ZA KUSHTUKIZA MKOANI MOROGORO

WAZIRI WA VIWANDA.BIASHARA NAUWEKEZAJI CHARLES MWIJAGE

WAKATI Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage  akijiandaa kuweka bayana orodha ya viwanda visivyofanya kazi leo, jana amefanya ziara ya kushtukiza katika viwanda vilivyobinafsishwa na serikali kwa wawekezaji mkoani Morogoro.
Ziara hiyo aliifanya katika kiwanda cha Moproco, ambako alieleza kufurahishwa na kasi ya utendaji wake huku akiahidi kutoa taarifa rasmi kwa viwanda vilivyokiuka agizo la serikali la kushindwa kufanya kazi miaka 20 tangu vibinafsishwe. Mwishoni wa wiki akiwa mjini Tanga, Rais John Magufuli alieleza masikitiko yake kuhusu Mwijage kushindwa kutekeleza maagizo yake ya kumtaka kunyang’anya viwanda vyote vilivyoshindwa kufanya kazi baada ya kubinafsishwa na kuvirudisha serikalini. Mwijage ameahidi kuweka kila kitu bayana leo mjini Dodoma.
Kiwanda cha Moproco kimeanza kuajiri wafanyakazi kwa awamu na kutokana na utendaji huo, waziri huyo alitumia fursa hiyo kuiagiza mamlaka za ukaguzi kufika kiwandani hapo ili kushauri taratibu mbalimbali ili zifuatwe. “Nimefika hapa kiwandani kujionea mwenyewe na nimefurahishwa na hatua ya kiwanda hiki cha Moproco kilivyoanza kufanya kazi na kuajiri wafanyakazi.
Wamefanya ukarabati wa mashine na hivi sasa uzalishaji wa mafuta umeanza hapa na hiki ndicho tunachotaka na viwanda vingine vifanye hivyo,” alieleza Mwijage. Waziri huyo pia alitembelea Kiwanda cha Morogoro Ceramic Wares Ltd, ambacho ni cha kuzalisha vyombo vya udongo vya matumizi ya majumbani zikiwemo sahani na vikombe na alikuta hakina mashine hata moja. Mbali na mashine zake kuondolewa ndani ya kiwanda hicho, pia alimkuta mlinzi pekee na wamiliki wake wakiwa hawajulikani walipo, kitendo kilichomchukiza na kueleza kuwa serikali sasa imechoshwa na hali hiyo.
Baada ya kumaliza ziara yake ya kushitukiza, Mwijage aliondoka eneo la viwanda la Kihonda na kuahidi kutoa tamko hilo la serikali akiwa Makao Makuu ya Nchi, Dodoma kuhusu viwanda vitakavyorudishwa serikalini baada kukiuka agizo la serikali. Naye Mkurugenzi wa Moproco, Talal Abood alisema uzalishaji huo umeanza mara baada ya kufanyika kwa marekebisho ya mashine zake zote.
Alisema walianza uzalishaji baada ya kufanya ukarabati mkubwa, ikiwemo kubadilisha mifumo ya mashine ili kukidhi viwango vya uzalishaji wa mafuta ya alizeti. Julai mwaka huu wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe, mkurugenzi huyo alisema uzalishaji wa hatua ya awali ulipangwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu na kutoa ajira za awali kwa wananchi kati ya 80 hadi 100.
Naye Kebwe ambaye alitembelea kiwanda hicho mapema Julai, alipongeza jitihada zilizofanywa na uongozi kwa kutekeleza maagizo ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kufufua viwanda vyote vilivyotolewa na serikali.


Akiwa hapo, alifahamishwa kuwa mashine zake zote ziliondolewa na kupigwa mnada kufidia deni la mkopo wa moja ya benki nchini. Kiwanda hicho kilichojengwa na Serikali ya Awamu ya Kwanza kwa ajili ya kuzalisha vifaa vya majumbani ambavyo ni vyombo vya udongo, masinki ya maji na vyoo, kilikuwa kinakidhi mahitaji ya ndani kutokana na malighafi yake kupatikana kwa wingi nchini.
Previous
Next Post »