JUMUIYA ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Meru mkoani Arusha, imesema ni marufuku wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari kwa wasichana kuvaa sketi fupi na wavulana kunyoa viduku, kuvaa suruali chini ya makalio ili kulinda na kutunza maadili ya Kitanzania.
Pia jumuiya hiyo imempongeza Rais John Magufuli kwa kupiga marufuku wazazi kuchangishwa michango mbalimbali kwa shule za serikali za msingi na sekondari nchini. Pongezi hizo zimetolewa jana na Mwenyekiti wa jumuiya hiyo wilayani Meru, Simon Kaaya jana wakati wa ziara yake ya kikazi alipotembelea shule za msingi na sekondari, kwenye Kata ya Ambureni.
Alisema baadhi ya shule walimu walikuwa siyo waadilifu ambapo walikuwa wanachangisha michango hiyo wakati mwingine hata kwa ajili ya chai za walimu. Kwa mujibu wa Kaaya, kuondolewa kwa michango hiyo kumesaidia wazazi kupata faraja kubwa na kuishukuru serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dk Magufuli anayehangaika na shida za wananchi wanyonge.
Kuhusu sare za shule za wanafunzi wilayani humo kutokidhi maadili ya kitanzania, Mwenyekiti huyo aliwataka wasimamie kikamilifu kuhakikisha hakuna wanafunzi wa kike wanaovaa sketi fupi za mlegezo au wavulana wanaovaa suruali mlegezo zilizobana miguuni pamoja na kunyoa kiduku. “Sisi kama wazazi jukumu letu kubwa ni kuhakikisha maadili mema yanazingatiwa haswa na watoto wetu kwa ajili ya kutunza heshima ya nchi yetu.
Tutaisimamia serikali wilayani hapa kuhakikisha inachukua hatua kali za kisheria dhidi ya wanafunzi wote wanaovaa nguo ambazo hazina heshima.” Alisema jumuiya ya wazazi moja ya jukumu lake kubwa ni kutoa malezi bora kwa jamii nzima ikiwemo watoto na vijana na kwamba ni jukumu lao kuhakikisha watoto na viajana wanakuwa na maadili mema katika jamii inayowazunguka.
ConversionConversion EmoticonEmoticon