China imeridhia kutoa msaada wa Dola za Marekani Milioni 62 sawa na Shilingi Bilioni 138.3 za Tanzania kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Usafirishaji hapa nchini.
Balozi wa China hapa nchini Wang Ke amesema hayo jana muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo na Rais Dkt John Magufuli na kumkabidhi barua yenye ujumbe wa Rais wa China Xi Jinping, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Balozi Wang Ke amesema msaada huo ni sehemu ya misaada na miradi mbalimbali ambayo China inaitekeleza hapa nchini Tanzania yenye lengo la kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati yake na Tanzania.
Kwa upande wake Rais Magufuli amemuomba balozi Wang Ke kumfikishia shukrani zake kwa Rais wa China kwa ujumbe na msaada huo ambao amesema utasaidia kuimarisha huduma za usafirishaji hapa nchini.
Wakati huo huo, Rais Magufuli amepokea taarifa kutoka kwa viongozi wa Shirika la Simu Tanzania kuhusu mwelekeo wa shirika hilo baada ya kuanza kutumika kwa sheria namba 12 ya mwaka 2017 ya Shirika la Simu Tanzania, iliyolibadili kutoka Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) na kuwa Shirika la Simu Tanzania (TTCL Corporation) kuanzia tarehe 01 Februari, 2018.
Pamoja na kupokea taarifa hiyo Rais Magufuli amemteua Dkt. Omari Rashid Nundu kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL Corp na Waziri Kindamba kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Corp, na amewataka kuchapa kazi kwa juhudi na kuhakikisha TTCL Corp inaongeza ufanisi, na kutoa gawio kwa Serikali.
Dkt. Omari Rashid Nundu na Waziri Waziri Kindamba wamemshukuru Rais Magufuli kwa uteuzi huo na wamesema TTCL itaendelea kujiimarisha kwa kupanua huduma za mawasiliano nchini, kuongeza na kuboresha bidhaa ikiwemo TTCL Pesa, kuzalisha faida zaidi na kuusimamia vizuri mkongo wa Taifa kwa maslahi na usalama wa nchi.
ConversionConversion EmoticonEmoticon