RAIS John Magufuli amefi chua ugumu, uliokuwa umegubika utekelezaji wa mradi wa upatikanaji wa pasipoti mpya za kusafi ria za kielektroniki huku akibainisha kuokolewa kwa mabilioni ya shilingi, yaliyolengwa kufanyiwa ufi sadi.
Akizungumza katika uzinduzi wa pasipoti hizo katika Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji jijini Dar es Salaam jana, Rais Magufuli alisema gharama za mradi huo wa pasipoti ni Sh bilioni 127.2 ambazo zote ni fedha za Serikali. Akimnukuu Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini, Dk Anna Makakala, Rais Magufuli alisema awali mradi huo ulipangwa kutekelezwa kwa Sh bilioni 400.
“Walipanga kupiga pesa za Watanzania, na ndiyo maana msishangae kwenye siku za nyuma kidogo kuna watu walizunguka sana na kupiga vita sana mchakato huu kwa sababu walijua wanataka kutengeneza shilingi bilioni 400, walijua Tanzania bado eneo la kuchuma,” alieleza Rais Magufuli. Alisema pasipoti hizo mpya, zitagharimu Sh 150,000 kila moja na zitatumika kwa miaka 10, kabla ya kuhuishwa tena.
Alisema matumizi ya pasipoti mpya za kielektroniki, yataondoa matumizi ya pasipoti za kawaida zinazotumika sasa. Kwa mujibu wa Rais Magufuli, pasipoti za kisasa zinakidhi viwango vya kimataifa kwa kuwa zina alama nyingi za kiusalama, na siyo rahisi kuzighushi licha ya gharama yake kutokuwa kubwa. “Pasipoti hii tunayoizundua leo ni ya kipekee sana, ni ya kielektroniki, ina alama nyingi za usalama.
Hii itasaidia kupunguza au kuondoa kabisa uwezekano wa kugushiwa, baadhi ya taarifa zake zinaweza kusomeka kwenye mifumo ya kielektroniki bila kulazimika kuipeleka pasipoti yenyewe, na hii itaokoa muda na itapunguza gharama,” alisema Rais Magufuli. AGIZO KWA UHAMIAJI Rais Magufuli aliitaka Idara ya Uhamiaji, kuhakikisha wananchi na wageni wanaoitembelea nchi wanapata huduma bora za uhamiaji na kwa haraka.
Alisema kwa kuwa katika kutekeleza mradi huo, wadau wote wanaohusika na masuala ya uhamiaji wakiwamo Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Mamlaka ya Vizazi na Vifo (Rita), Polisi, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni Tanzania (Brela), Mamlaka ya Mapato (TRA), Bodi ya Utalii na Idara ya Wakimbizi, wameshirikishwa na kutakuwa na mfumo wa mawasiliano, hivyo hatarajii kuona wananchi wanatumia muda mwingi kabla ya kupata pasipoti zao.
“Nitashangaa pia kama malalamiko ya upatikanaji Visa yataendelea kusikika kama ilivyotokea wakati wa sherehe za waumini wa madhehebu ya Bohora na wakati wa ujio wa Timu ya Everton mwaka jana. “Nitashangaa kama vibali vya ukaazi vitatolewa kiholela na kwa watu wasio na sifa; nitashangaa kama ukusanyaji mapato hautaongezeka,” alieleza Rais Magufuli.
Aidha, aliitaka Idara ya Uhamiaji kuwa makini katika masuala yanayohusu usalama na uraia wa nchi wakati wanapotekeleza mradi huo. Aliwataka kuzingatia uaminifu na uadili kwa kuwa pamoja na kuwa na mfumo wa kisasa wa Uhamiaji Mtandao, ufanisi wake utategemea utendaji kazi na uadilifu wa watumishi wa Idara hiyo. Rais aliwataka watendaji wa idara hiyo kuepuka vitendo vya rushwa na kwa watumishi watakaobainika kujihusisha na rushwa wafukuzwe kazi.
UHAMIAJI MTANDAO Rais alisema kuzinduliwa kwa pasipoti mpya ni ishara ya kuanza utekelezaji mkubwa wa Uhamiaji Mtandao (e- Immigration) utakaotekelezwa kwa awamu nne.
Alisema baada ya uzinduzi, awamu itakayofuata itakuwa ni kufunga mfumo wa Visa wa kielektroniki (e-visa), Hati za Ukaazi za Kielektroniki, usimamizi wa mipaka kwa njia ya kielektroniki na awamu ya nne itahusu kupanua huduma za uhamiaji mtandao kwenye ofisi za balozi za Tanzania na wilaya zenye shughuli nyingi za uhamiaji. UBALOZI WA IRELAND Aliushukuru Ubalozi wa Ireland nchini kwa kazi kubwa waliyoifanya mpaka Serikali ya nchi hiyo, kukubali kuidhamini Tanzania katika mradi huo.
Alisema kupitia Ubalozi huo kuliweza kupatikana kwa Kampuni ya HID Global ya Marekani iliyokubali kutengeneza pasipoti hizo kwa gharama ya Sh bilioni 127.2 badala ya Sh bilioni 400. MAKAO MAKUU UHAMIAJI DODOMA Baada ya Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk Makakala kumshukuru Rais kwa kuwapatia nyumba 103 mjini Dodoma za wafanyakazi wa Uhamiaji pamoja na kumweleza azma ya Makao Makuu ya Idara hiyo kuhamia Dodoma, Rais Magufuli aliahidi kutoa Sh bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi hizo mjini humo.
Mbali na ahadi hiyo, Rais pia aliwahakikishia Uhamiaji kuwa changamoto zao zikiwemo vitendea kazi, vifaa mbalimbali na nyinginezo atazishughulikia. VIONGOZI WAPATIWA PASIPOTI MPYA Baada ya kuzindua Pasipoti hizo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Mwigulu Nchemba alitumia fursa hiyo kuwapatia viongozi mbalimbali pasipoti mpya za kielektroniki.
Viongozi waliopatiwa pasipoti hizo ni Rais Magufuli, Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk Mohamed Shein, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Viongozi wengine ni Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Amani Abeid Karume, Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma, Jaji Kiongozi Ferdinand Wambali na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson. Wengine ni Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, Mbunge wa Muheza, Adadi Rajab na Mbunge wa Ilala Mussa Azan Zungu.
ConversionConversion EmoticonEmoticon