MABALOZI 11 wanaziwakilisha nchi zao nchini Kenya wametoa mwito kwa kiongozi wa umoja wa vyama vya upinzani (NASA), Raila Odinga kutambua mamlaka ya Rais Uhuru Kenyatta.
Taarifa ya mabalozi hao imesema, demokrasia ya nchi hiyo ipo njia panda na wametoa mwito kwa Rais Kenyatta kuzingatia utawala wa sheria na asiingilie uhuru wa vyombo vya habari au kuwanyanyasa wapinzani.
Walionya kwamba, kama Serikali na wapinzani wakiendelea kukiuka sheria Kenya itaingia kwenye mgogoro wa kisiasa. Mabalozi hao pia wamemuonya Odinga kuwa, akiendelea kutoutambua uongozi wa Kenyatta na Naibu Rais William Ruto, ataharibu kumbukumbu yake.
Kwa mujibu wa taarifa ya wanadiplomasia hao wakiongozwa na Balozi wa Marekani nchini Kenya, Robert Godec, hawaridhishwi na siasa za sasa nchini humo ikiwa ni pamoja na ‘kuapishwa’ kwa Odinga, kukamatwa kwa wapinzani na kuingiliwa kwa vyombo vya habari.
Januari 30 asubuhi serikali ya Kenya ilizima matangazo ya vituo vinne vya televisheni, na siku chache baadaye, Wakili aliyedaiwa kumuapisha Odinga, Miguna Miguna alifukuzwa nchini humo akidaiwa kuwa si raia.
Taarifa hiyo iliyosainiwa na Balozi Godec na mabalozi wengine kutoka nchi za Ulaya imetoa mwito kwa Odinga kuitambua Serikali ya Kenyatta ili kuwezesha kufanyika kwa mazungumzo ya wazi ya kitaifa kujadili masuala ya muda mrefu yanayolikwaza taifa hilo.
Mabalozi hao wameionya NASA iache kusababisha vurugu au kuchukua madaraka kwa njia zisizo za kikatiba. Kwa mujibu wa wanadiplomasia hao, hawataingilia masuala ya ndani ya Kenya.
ConversionConversion EmoticonEmoticon