Kampuni ya uwindaji yamjibu Maghembe

KAMPUNI ya Wengert Windrose Safaris (Tanzania) Limited (WWS), imesema kauli iliyotolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe kwamba Mahakama Kuu ilitoa amri kwa waziri ikimtaka kuirudishia Green Miles Safari Co. Limited (GML) kibali cha uwindaji na kitalu ambacho kinaendeshwa na WWS sio za kweli.
Taarifa ya WWS iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari ilifafanua kuwa hakuna uamuzi wowote uliotolewa na Mahakama ukitamka au kuamua kwamba GML ndio mmiliki halali wa kitalu cha uwindaji ambacho sasa kinaendeshwa na WWS.
Waziri Maghembe alitoa kauli hiyo wiki iliyopita wakati anajibu hoja za wabunge bungeni. Kampuni hiyo pia ilisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa Mahakama haikuwahi kuamuru Wizara ya Maliasili na Utalii kuirudishia GML leseni ya uwindaji na vitalu vya uwindaji vilivyonyang’anywa kutokana na maofisa wake kudaiwa kushiriki uwindaji haramu katika pori la uwindaji la Selous.
Taarifa hiyo ilifafanua kwamba ukweli kuhusu jambo hilo ni kwamba Agosti 28, WWS ndio ilifungua shauri la madai Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara dhidi ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na GML.
Ilieleza kuwa katika shauri hilo WWS ilikuwa ikipinga uamuzi wa waziri kubadilisha jina la kitalu kinachoendeshwa na WWS ili kutoa mwanya wa kitalu hicho kupewa GML. “Walalamikiwa wote hao hawakuwasilisha utetezi wao mahakamani.
WWS imeshtushwa na kauli ya Waziri wa Maliasili na Utalii kwamba Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara ilitoa amri kwa waziri ikimtaka kuirudishia GML kibali cha uwindaji na vitalu vya uwindaji. Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara haijawahi kutoa uamuzi kama huo.
“Vilevile tumesikitishwa na kauli ya Waziri kwamba WWS ilikataa kuhama katika kitalu hicho kwa madai kwamba kitalu hicho ndicho kilikuwa bora zaidi na kwamba ilikuwa imewekeza zaidi katika kitalu hicho, hivyo isingekuwa tayari kuhama hata kama Serikali haikuipa kitalu hicho.
“Tunasema kwamba kauli hiyo si ya kweli. Kampuni ya WWS haijawahi kutoa kauli kama hiyo mahali popote au kwa mtu yeyote. Tunasema kwamba WWS iliiomba wizara kitalu hiki kwa kipindi cha mwaka 2013 - 2018 na wizara ikaipa kampuni yetu kitalu hiki,” ilisema taarifa hiyo.
WWS ilifafanua kuwa ililazimika kufungua shauri la madai Na. 113 la mwaka 2013 katika Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara kupinga kitendo cha Waziri kutaka kuwanyang’anya kitalu hicho baada ya kuwa wameshapewa kwa kisingizio cha kubadilisha jina la kitalu.
“Shabaha ya kubadilisha jina la kitalu ilikuwa imelenga kuipokonya kampuni yetu kitalu hiki baada ya kuwa tumemilikishwa kihalali na Serikali,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo. Taarifa ilifafanua kuwa tangu kupewa kitalu hicho mwaka 2013, Serikali imewawekea notisi za kulipa ada za vitalu kwa jina la Lake Natron Controlled Area kama ilivyokuwa siku zote, na wameendelea kulipia ada za kitalu hicho kwa Serikali kwa kutumia jina hilo hilo tangu mwaka 2013 hadi leo hii.
Taarifa iliongeza kuwa serikali imewapa vibali vya kuendesha shughuli zao kama kupeleka wageni na wafanyakazi wao kuingia humo kwa kutumia jina hilo.
Previous
Next Post »