Polisi yataka ushirikiano kuushinda uhalifu

KAMANDA WA POLISI MKOANI ARUSHA
CHARLES MKUMBO
JESHI la Polisi limesema haliwezi kuushinda uhalifu nchini peke yake, bali kwa ushirikiano kutoka kwa viongozi wa dini, wanasiasa na wananchi kwa ujumla. Rai hiyo ilitolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo mwishoni mwa wiki katika kikao ambacho kiliwashirikisha viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali pamoja na madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa nia ya kuimarisha amani na usalama.
Mkumbo alisema Jeshi la Polisi pekee haliwezi kukabiliana na uhalifu bali kwa kushirikiana na viongozi wa dini na wa kisiasa na wananchi, ndio wataweza kuushinda uhalifu. “Sote tuna jukumu la kufichua uhalifu na wahalifu kupitia taarifa za waumini wetu hasa kwa viongozi wetu wa dini kuendelea kuhubiri na kutoa mawaidha katika makanisa na misikiti, huku madiwani waendelee kufanya hivyo katika maeneo yao ya kiutawala hasa wanapokutana na wananchi kwenye mikutano mbalimbali,” alisema.
Naye Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro alisema wananchi pamoja na viongozi wote wasiwe na hofu kwa kuwa Jiji la Arusha linaongozwa na Chadema kwani wao kama viongozi wa siasa wanahitaji amani na wanalitambua jukumu hilo.
Naye Shehe wa Wilaya ya Arusha, Abraham Salum alisema kikao hicho kimekuja wakati muafaka kwani mikoa ya Tanga na Mwanza kumejitokeza vitendo vya uvunjifu wa amani, matukio ambayo hapo awali hayakuwepo nchini na kulishauri jeshi hilo kuongeza weledi katika kupambana na uhalifu na akiwataka wananchi kutoa ushirikiano.
Akichangia mjadala huo, Padri Festus Mangwangi wa Parokia ya Mtakatifu Theresia ya Kanisa Katoliki, alisema wao wana dhamana kubwa ya kulisaidia Jeshi la Polisi katika kuhubiri amani kupitia waumini wao, na kuwa amani iliyopo idumishwe kwani baadhi ya nchi zina vurugu na zinatamani amani iliyopo nchini mwetu
Previous
Next Post »