MGONJWA mmoja aliyekuwa akiugua ugonjwa wa ajabu, ulioukumba mkoa wa Dodoma, amefariki na kufanya idadi ya waliokufa kwa ugonjwa huo kufikia saba huku wanaougua wakiongezeka na kufikia 21, kati ya hao wawili ambao ni watoto wakiwa katika hali mbaya.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema hayo mjini hapa jana alipotoa taarifa kuhusu hali ya ugonjwa huo na hatua ambazo serikali imekuwa ikichukua kukabiliana nao.
Ugonjwa huo kwa mjibu wa Ummy, ulianzia katika wilaya ya Chemba ambako watu tisa wa familia moja kutoka kijiji cha Mwaikisabe kata ya Kihama, waliathirika na baadaye wagonjwa wengine walianza kupatikana kutoka vijiji vya karibu.
Dalili za ugonjwa huo zilionekana kuwa ni kutapika, kuharisha, kupata rangi ya manjano machoni, kuwa na maumivu ya tumbo na kuvimba tumbo kwa kujaa maji katika muda mfupi, lakini hawapati joto kali wala harara katika ngozi.
Taarifa za awali za chanzo cha ugonjwa huo kwa mujibu wa Waziri, ilitajwa kuwa ni watu hao kula nyama ya ng’ombe aliyechinjwa baada ya kuvunjika mguu, ingawa baaadhi ya watu waliokula nyama ya ng’ombe huyo hawajaugua.
Katika familia hiyo ugonjwa huo unaoshika watoto kwa watu wazima, pia uliua mbwa wakubwa watatu, mbwa wadogo watatu na paka mmoja. Akizungumzia uchunguzi wa awali uliofanywa na Maabara Kuu ya Taifa, Ummy alisema umeonesha kuwa si homa ya manjano wakati vipimo vingine vikifanyika kuona kama ni Homa ya Bonde la Ufa, huku kesho Ofisi ya Mkemia Mkuu ikitarajiwa kutoa matokeo ya uchunguzi wake.
Tathmini ya taarifa hizo za awali, Ummy alisema inahusisha ugonjwa huo na ulaji wa vyakula vyenye sumu kuvu, ambayo hupatikana katika vyakula vya aina mbalimbali visivyohifadhiwa vizuri.
Waziri huyo alisema pia tathmini hiyo imebaini kuwa ugonjwa huo si kimeta kwa kuwa hauambukizi, ila unaonekana unaweza kuwa umetokana na matumizi ya kitu ambacho ni maarufu kwa kundi hilo la watu.
Tayari kwa mujibu wa Ummy, sampuli za nafaka walizokuwa wakitumia familia zilizoathirika zimechukuliwa, kwa ajili ya uchunguzi zaidi ngazi ya Taifa katika Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Maabara ya Mkemia Mkuu na leo mchana, huenda TFDA ikatoa majibu ya uchunguzi wake.
Mbali na sampuli za nafaka walizokuwa wakitumia familia za waathirika, Ummy alisema sampuli za damu ya wagonjwa, kinyesi, matapishi, vinyama vitokanavyo na ini, zimechukuliwa na kupelekwa katika maabara.
Wagonjwa hao kwa sasa wanahudumiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma katika wodi maalumu, huku timu ya awali ya uchunguzi ikiwa imepelekwa katika wilaya za Chemba na Kondoa kwa uchunguzi.
Jana timu nyingine ya wataalamu iliwasili kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Ofisi ya Mkemia Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na TFDA kwa ajili ya kuongeza nguvu.
ConversionConversion EmoticonEmoticon