Pwani wapata bilioni 18/- kwa kuuza korosho


MKOA wa Pwani umefanikiwa kukusanya zaidi ya Sh bilioni 18 kutokana na mauzo ya zao la korosho kwa msimu wa 2015/2016.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo, mjini Mkuranga juzi.
Alisema hayo katika mkutano wa Tathmini ya mfumo wa stakabadhi ghalani msimu uliopita na mikakati ya kuboresha mfumo huo katika msimu wa mwaka 2016/2017.
Ndikilo alisema jumla ya tani 7,885.9 za korosho zilikusanywa na kuuzwa na wakulima msimu huo uliopita. Alisema tani 3,490.5 daraja la kwanza ziliuzwa kwa wastani wa bei ya Sh 2,613.3 kwa kilo na bei ya juu ilikuwa Sh 2,900 kwa kilo.
“Korosho daraja la pili ziliuzwa kwa wastani wa shilingi 2,453 kwa kilo na bei ya juu ikiwa shilingi 2,500 kwa kilo ambapo mfumo huo umesababisha kufanikiwa kupata mapato makubwa kwa msimu huo,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa hata wataalamu na wakulima, wamekiri haijawahi kutokea bei kama hiyo kwa korosho. Walisema bei hiyo imewapa manufaa wakulima mkoani Pwani na kuongeza pato lao kimaisha.
Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho nchini, Anna Abdallah alisema mfumo wa stakabadhi ghalani ni mkombozi kwa wakulima.
Alisema anawashangaa wale wanaobeza mfumo huo.
Abdallah alisema kuwa mfumo huo unakuza soko la korosho nchini, licha ya kuwepo changamoto chache, ikiwemo kuhakiki ubora wa korosho kwenye maghala. Aliwataka wakulima kuzingatia ubora wa korosho.
Previous
Next Post »