Mabasi ya city boy 12 yasitishiwa safari


MABASI 12 ya Kampuni ya City Boy yamefungiwa kutoa huduma wakati mamlaka zikiendelea na uchunguzi wa ajali zilizotokea kabla ya kuja na hatua kamili.
Aidha, madereva wawili wa mabasi ya City Boys waliosababisha ajali juzi mkoani Singida na kusababisha vifo vya watu wapatao 30, watafunguliwa mashitaka ya kuua bila ya kukusudia na si makosa ya usalama barabarani kama ilivyozoeleka.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Thobias Sedoyeka alimtaja Jeremiah Martin (34) aliyekuwa akiendesha gari namba T 531 BCE lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Kahama kwamba anashikiliwa na polisi. Dereva mwingine, Martin Mwakalukwa inasadikiwa kuwa alitoroka mara baada ya ajali na anatafutwa na polisi.
Wakati mamlaka zikiendelea na mchakato huo wa kuadhibu waliosababisha vifo hivyo, taarifa kutoka mkoani Singida na Dodoma waliko majeruhi na miili, zinaonesha hadi jana maiti walishatambuliwa.
Mathalani, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma walijitokeza watu wengi kutambua ndugu zao, akiwemo mmoja ambaye alitaja familia ambayo mume, mke na mtoto walipoteza maisha kwenye ajali hiyo wakati mumewe akimpeleka nyumbani kwao kumtambulisha kwa wazazi.
Mabasi yafungiwa
Uamuzi wa kufungia mabasi hayo sanjari na mengine ya kampuni za Mohamed Trans, OTA na Super Sami umechukuliwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra).
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Sumatra, Gilliard Ngewe alisema magari hayo yamefungiwa kwa mujibu wa kifungu namba 15 cha Sheria ya Sumatra namba tisa ya mwaka 2001.
Ngewe alisema kampuni ya Mohamed Trans imefungiwa kutoa huduma kwa sababu ya uchakavu wa mabasi yake ambayo yamekuwa yakichelewa kufika vituoni na kampuni hizo nyingine ni kutokana na mabasi yake kusababisha ajali.
Alifafanua magari ya City Boy yaliyofungiwa kuanzia jana ni yanayofanya safari kati ya Dar es Salaam na Kahama (Shinyanga), Karagwe (Kagera), Handeni (Tanga) na Mwanza.
Alitaja namba za usajili za magari ya Kampuni City Boy yaliyofungiwa kuwa ni T 531 DCE, T 528 DCE, T 661 DGG, T 383 CSV, T 280 DCN, T 279 DCN, T 662 DGG, T 445 CSV, T 247 DCD, T 983 DCE, T 846 CUB na T 903 CPD. Alisema kampuni zote tatu (Ota, Super Sami na City Boy) zimesababisha vifo vya watu 46 na majeruhi 73 kwa kipindi cha wiki moja.
‘’Tumeyafungia mabasi haya hadi uchunguzi utakaofanywa kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kuhusu vyanzo vya ajali hizi utakapokamilika kwa sababu tukiyaacha yataharibu upelelezi wetu na baadaye tutawachukulia hatua za kisheria kwa kuwapeleka madereva waliosababisha ajali hizi mahakamani,’’ alisema Ngewe.
Alisisitiza kuwa mabasi hayo hayataruhusiwa kuendelea kutoa huduma za usafiri njia hizo hadi mamlaka hiyo itakapopokea taarifa za ukaguzi zinazothibitisha kuwa mabasi hayo yanakidhi viwango vya ubora kwa kuwa na madereva wenye sifa.
Pia alisema wanatilia shaka sifa za madereva wa mabasi ya City Boy kwa kile walichoeleza kuwa wamekuwa na mazoea ya kufanya mizaha wanapopishana wakiwa safarini. Ajali ya mabasi ya City Boy yenye namba za usajili T 531 DCE na T 247 DCD, ilisababisha vifo vya watu 30 na majeruhi 54.
Madereva kushitakiwa
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga alisema madereva wawili waliosababisha ajali hiyo, watafunguliwa mashitaka ya kuua bila kukusudia kwa sababu ajali hiyo sio ya kawaida.
Alisema basi la kampuni ya City Boy lililokuwa likitoka Dar es Salaam; ambalo lilihusika katika ajali hiyo, kabla ya ajali lilikamatwa Singida Mjini likiwa kwenye mwendokasi wa kilometa 122 kwa saa na dereva aliandikiwa faini ya Sh 30,000.
“Ajali hii haikuwa ya kawaida ni tukio la kufanya mauaji bila ya kukusudia. Tunadhamiria kuwafikisha mahakamani madereva wa magari haya ya City Boy kwa tuhuma hizo,” alisema Mpinga. Akielezea ajali zilizotokea wiki hii, Kamanda Mpinga alisema Super Sami lilipata ajali Juni 28 mwaka huu, saa 8 usiku katika Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.
Lilikuwa likitoka Shinyanga kwenda Mwanza kabla ya kuacha njia na kupinduka na kusababisha vifo vya watu watano na majeruhi 13. Pia Julai mosi mwaka huu, maeneo ya Veta Dakawa katika barabara ya Dodoma- Morogoro, malori mawili yaligongana na kuwaka moto na kusababisha vifo vya watu watano.
Vile vile, alieleza kuwa eneo hilo hilo Juni 2, basi la Kampuni ya OTA lilipata ajali kwa kugonga mabaki ya malori hayo na kusababisha vifo vya watu sita na majeruhi sita.
Abiria, wamiliki walaumiwa
Alifafanua kuwa ajali hizo zimechangiwa na baadhi ya abiria wanaoshabikia mwendokasi na wamekuwa hawatoi taarifa za madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani. Alisema abiria wengi wanasubiri ajali itokee ndipo waseme dereva alikuwa anaendesha kwa mwendokasi.
Aidha, alisema zipo taarifa kwamba baadhi ya wamiliki wa mabasi wamekuwa chanzo cha madereva wao kuendesha kwa mwendokasi kwa kuwa wanawapa motisha pale wanapowahi kufika vituo vya mwisho wa safari .
Alisema pia wamekuwa wakiwalipia faini wanapokamatwa kwa kuendesha kwa mwendo huo. “Kwa uchunguzi wa awali, ajali zote zimechangiwa na uzembe wa madereva pamoja na mwendokasi. Ni dhahiri madereva wamekuwa wakikiuka kwa makusudi sheria inayowataka kuendesha kwa mwendo usiozidi kilometa 80 kwa saa,” alisisitiza Mpinga.
Hata hivyo, alisema Polisi na Mamlaka zinazosimamia Usalama Barabarani wataendelea kuchukua hatua kali kwa madereva na wamiliki wasiotaka kuzingatia sheria na kanuni za Usalama barabarani.
Maiti watambuliwa
Jumla ya miili 13 kati ya 28 ya waliofariki kwa ajali ya mabasi ya City Boy iliyotokea juzi katika eneo la Maweni wilaya ya Manyoni mkoani Singida imetambuliwa.
Mamia ya wananchi kutoka mkoani Dodoma na mikoa jirani jana walikusanyika nje ya chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma kwenda kutambua ndugu zao waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk Ibenze Ernest alisema maiti 13 kati ya 30 ndiyo wametambuliwa.
“Maiti nyingi hazijatambuliwa kwa sababu mbalimbali ikiwemo kuumia vibaya na kuondoa muonekano wao halisi huku wengine wakiwa wamegawanyika viwiliwili na vichwa,” alisema.
Majina ya waliokufa, majeruhi
Dk Ibenze aliwataja marehemu waliotambuliwa kuwa ni Ismail Bashe, John Lukanda, Paul Mfaume, Dickles Kwabugili, Rabia Lema na Levoso Israel. Wengine ni Paulina Martine, Resta Exavery, Kefun Deus, Charles Mamunyi, Betty Zumbe, Jesca Lazaro na Leonard Chacha.
Sababu za kutotambuliwa
Mganga mkuu huyo alisema maiti wengi hawakutambuliwa kwa sababu mbalimbali, ikiwemo kuumia vibaya na kuondoa mwonekano wao halisi huku wengine wakiwa wamegawanyika viungo.
“Sababu ya kutotambuliwa kwa idadi kubwa ni kutokana na ndugu wengi kutofika, kuumia vibaya lakini pia vichwa vingi vipo peke yake na miili ipo peke yake,”alisema.
Aidha, aliwataja majeruhi saba wanaendelea kupatiwa matibabu kuwa ni Katra Abubakari (12) ambaye amevunjika miguu yote na amelazwa wodi ya wagonjwa mahututi.
Majeruhi wengine ni Athuman George mkazi wa Geita, Jamila Mathias mkazi wa Shinyanga, Monza Labani mkazi wa Nzega na Disko Wabare mkazi wa Kahama ambaye ni Katibu wa Wazazi wa CCM wilaya ya Kahama.
Mwingine ambaye hajatambulika pia amelazwa wodi ya wagonjwa mahututi mwingine ametambuliwa kwa jina moja la Mujaidi. Alisema majeruhi waliowapokea hospitalini hapo ni 15 ambao baadhi walitibiwa na kuruhusiwa.
Watano walifanyiwa upasuaji kutokana na mahitaji ya matibabu yao. Dk Ibenze ambaye ni Daktari Bingwa wa Mifupa alisema majeruhi kuchelewa kufikishwa hospitalini ni changamoto waliyokutana nayo.
Simulizi za ndugu
Mmoja wa watu waliofika kutambua maiti wa ajali hiyo jana alasiri, Said Musa mkazi wa Dodoma alisema alitambua ndugu watatu wa familia moja.
“Mwanaume aliyekufa na familia yake anafahamika kwa jina la Peter Sinton na mkewe namfahamu kwa jina moja la Rose ila sijui jina la mtoto,” alisema.
Alisema Peter alikuwa mwalimu katika shule ya Sekondari Mtibwa mkoani Morogoro na alikuwa akitokea mkoani Tabora kumtambulisha mkewe kwa wazazi wake.
Hadi jana mchana, miili yote ilikuwa imehifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya Rufaa ya Dodoma wakati utambuzi ukiendelea.
Previous
Next Post »