Mamlaka ya mawasiliano nchini Tanzania TCRA imezipiga faini ya zaidi ya dola laki tatu $300,000 makampuni sita ya simu nchini humo kwa kukiuka sheria katika utoaji huduma zao za kimawasiliano.
Mkuu wa tume mamlaka ya mawasiliano nchini Tanzania TCRA James Kilaba amesema kuwa makampuni hayo ambayo ni Airtel Tanzania Limited, SMART, TIGO, Halotel, Vodacom Tanzania Limited na Zantel yanatakiwa kulipa faini hiyo ifikapo Julai 31.
TCRA imetoa siku saba kwa kampuni hizo za simu kuzima laini zote zilizokiuka masharti ya usajili zilizoko sokoni.
Akizungumza mjini Dar es Salaam bw Kilaba alisema hatua hiyo ''imetokana na mamlaka hiyo kufanya ukaguzi katika mifumo ya usajili wa laini za simu na kugundua baadhi ya namba zinazohudumu hazijasajiliwa majina, nambari za vitambulisho na nyaraka zingine muhimu''.
“ TCRA imebaini baadhi ya kampuni hizo hazijafunga namba za simu hadi usajili ukamilike hiyo ikiwa ni kinyume cha kanuni ya 33 ya Leseni za mwaka 2011 zilizotolewa chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2010.
Sheria ya EPOCA ya 2010 inazitaka kampuni zinazotoa huduma za simu kusajili laini zote kwenye mirandao yao ili kumlinda mtumiaji kutokana na matumizi mabaya ya huduma za mawasiliano, kuwawezesha kuwatambua watumiaji wa huduma za ziada za simu na kuimarisha usalama wa taifa.
Mamlaka ya mawasiliano Tanzania inayalalamikia makampuni hayo kwa kukiuka sheria kwa kuruhusu kadi za simu ambazo hazijasajiliwa kufanya kazi.
Hata hivyo makampuni hayo ya simu yameagizwa kuzifunga mara moja kadi za simu ambazo hazina usajili ama usajili wake una utata.
Hivi karibuni Tanzania imeungana na nchi nyingine za Afrika kwa kuzima zaidi ya simu milioni na laki saba, huku simu zaidi ya laki moja na elfu kumi zikiwa hazina namba halisi ya utambulisho yaani IMEI.
ConversionConversion EmoticonEmoticon