RAIS John Magufuli amesema wakurugenzi watendaji (DED) wa halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji aliowateua hivi karibuni, hakuwachagua kwa kubahatisha wala hakuchagua vilaza.
Pamoja na hayo, Magufuli ametoboa siri ya kuihamishia Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) chini ya Ofisi ya Rais kuwa ni baada ya kubaini miaka ya nyuma nafasi za ukurugenzi zilikuwa zinatolewa kwa ushawishi na rushwa.
Rais alisema hayo Ikulu Dar es Salaam jana katika hafla fupi ya viongozi hao wapya ya kula kiapo cha Uadilifu wa Uongozi wa Umma kupitia Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na kupatiwa semina ya maadili ya viongozi wa umma.
Alisema tangu awateue wakurugenzi hao kumekuwa na maneno ya chinichini na mitandao ya kijamii, ikidai kuwa wengi wao hawana sifa na kufikia hatua ya kumtaja Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Wilaya ya Itigi mkoani Singida, Pius Shija Luhende kuwa ni mhudumu wa hoteli iliyopo Sinza jijini Dar es Salaam.
Ma-DED wana sifa za kutosha
“Lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ni kuwatumikia wananchi na kutimiza ahadi pamoja na Ilani ya CCM ya mwaka 2015 kwa kipindi cha miaka mitano. Tayari hadi sasa miezi minane imeshapotea, nataka utekelezaji wa ahadi hizi uende kwa kasi ya ajabu… “…Sasa kwa kasi hii ninayoitaka siwezi kubahatisha katika uteuzi wa viongozi watakaofanikisha azma hii. Hawa wakurugenzi niliowachagua asilimia 80 wana Shahada ya Uzamili na wengine wana Shahada na uzoefu wa kutosha,” alisisitiza Rais Magufuli.
Kuhusu uteuzi wa Shija, alisema anafahamu kuwa mkurugenzi huyo ana sifa za kutosha kuitumikia nafasi hiyo kwa kuwa ana Shahada ya Uzamili na Stashahada na alikuwa ni mkaguzi wa shule.
“Unajua baada ya hili la mitandao ya kijamii nimejifunza mengi, ukiona adui anakushangilia ukifanya jambo, rudi nyuma ujiulize umekosea wapi lakini ukiona adui yako anakushambulia basi ujue umemtwanga,” alisema Rais Magufuli.
Alisema anafahamu kuwa nafasi ya ukurugenzi wa halmashauri ni muhimu katika kujenga uchumi hasa wa chini ndio maana katika kuwateua viongozi hao, ametumia takribani miezi minne kuwachuja na kuwachambua ili kupata viongozi wenye sifa na vigezo stahili.
Hongo kupata u-DED
Alisema zamani wakurugenzi wengi walikuwa wakipata nafasi hiyo kwa kufanya ushawishi kwa kushirikiana na maofisa wa Tamisemi na kuwahonga fedha.
“Pale Tamisemi kulikuwa na timu imejipanga kufanikisha hili. Nimeshaagiza waziri ahakikishe watu wote waliohusika kwa hili wanaondolewa ndio maana niliamua wizara hii iwe chini yangu kwa makusudi,” alifafanua.
Akizungumzia uwajibikaji wa wakurugenzi hao, alisema fedha nyingi za serikali hupelekwa kwenye halmashauri, eneo ambalo limekuwa na sifa mbaya ya fedha hizo kutumika hovyo bila kuzingatia weledi na maadili.
Alisema ndio maana katika uteuzi wa wakurugenzi hao kati ya wakurugenzi 185 waliokuwapo, wa zamani walioendelea ni 60 pekee na 120 ‘wametemwa’, hali inayodhihirisha kuwa waliobaki ni watendaji wazuri ambapo yeye aliwaita ‘majembe’.
Alisema kila mkurugenzi Aliwataka kuhakikisha wanazisimamia vyema fedha za serikali zinazowasilishwa katika halmashauri na kuepuka kuburuzwa, kujipendekeza, kukejeliwa au kutumika vibaya kwa kuingia mikataba na kampuni feki zisizoweza kutekeleza vyema wajibu wake.
Fedha za Mfuko wa Barabara
Magufuli alisema anazo taarifa za baadhi ya wakurugenzi, walikuwa wakishirikiana na mameya, madiwani na wenyeviti wa halmashauri kwa kupitisha na kuingia mikataba na kampuni zilizo na uwezo chini ya viwango katika kutekeleza miradi ya barabara; na matokeo yake miradi mingi haikuwa na mafanikio.
“Nawaambieni mkisimamia maadili hakuna atakayewafukuza kazi. Msijipendekeze kwa mtu kwa sababu hakuna aliyepenyeza majina yenu kwangu hadi mkachaguliwa. Kuna mmoja jina lake lilipenyezwa nikalitupilia mbali,” alisema.
Fedha za elimu bure
Aliwataka kuwa makini na kusimamia vyema Sh bilioni 18.77 zinazotolewa na serikali kila mwezi kwa ajili ya elimu bure katika shule za msingi na sekondari kwa kuhakikisha zinatumika vyema kwa lengo lililokusudiwa.
Alisema wapo wakurugenzi waliokuwa wakizitumia vibaya fedha hizo kwa madai kuwa ni nyingi, huku kukiwa na taarifa za baadhi ya walimu wakuu katika kufanya udanganyifu kwa kuandika orodha ya uongo ya wanafunzi na kuongeza idadi ili wapate mgawo mkubwa wa fedha hizo.
Matumizi ya EFDs serikalini Pamoja na hayo, Rais Magufuli aliziagiza wizara zote nchini chini ya makatibu wake wakuu na halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji na taasisi zote za serikali, kuhakikisha wanaanza mara moja kukusanya mapato yake kwa kutumia mashine za kielektroniki (EFDs).
“Haiwezekani mfanyabiashara alazimishwe kutumia mashine hizi wakati sisi serikalini tunakusanya mapato yetu bilaaliyechaguliwa, atambue kuwa sifa zake zilichambuliwa na Rais mwenyewe. “Ndio maana mimi sitembei, nilikuwa nalala saa sita hadi saa nane usiku, nawafahamu wote kwa sifa hadi majina, ninaamini hawataniangusha,” alisema.
kutumia mashine za EFDs. Ninawataka nyie wakurugenzi mliopo hapa mkifika katika maeneo yenu mhakikishe halmashauri zenu zinakusanya mapato yake kwa kutumia EFDs,” alisisitiza.
Aidha aliwaagiza wakurugenzi hao kuhakikisha wanashiriki katika kutimiza ndoto ya Tanzania kuwa taifa lenye kipato cha kati kupitia uchumi wa viwanda kwa kila mmoja kuhakikisha katika eneo lake kunaanzishwa viwanda vidogo.
Kodi ndogo ndogo
Akizungumzia kero na changamoto zinazowakabili wananchi, Dk Magufuli aliwataka wakurugenzi hao kuhakikisha kipaumbele chao kikubwa kinakuwa ni kuondoa kero za wananchi hasa wale wenye maisha ya chini.
Alisema watanzania wamekuwa wakiteseka kwa muda mrefu na kuhangaishwa na kodi za ajabu hali iliyochangia kurudisha maisha yao nyuma.
“Unakuta mtu analima mpunga wake, akivuna na kuubeba kuupeleka nyumbani kwa matumizi anadaiwa kodi, mbona wakati analima hamkudai kodi? “Nawaomba mhakikishe kodi za aina hii mnazizuia kwani Serikali hii wakati ikiomba kura ya kuingia madarakani, haikuahidi kutengeneza kero kwa wananchi bali kuziondoa kero hizo,” alisema.
Kutumbua majipu
Aliwaagiza wakurugenzi hao watakapofika kwenye vituo vyao vya kazi, kuhakikisha wanachukulia hatua na kuwaondoa mara moja watendaji walio kwenye mamlaka yao wasiowajibika na wale wanaofanya kazi kwa kujifanya miungu watu.
“Nina taarifa wapo watendaji kata ambao wanajifanya miungu watu, kazi yao kubwa ni kuichonganisha Serikali na wananchi, tumieni madaraka yenu kuwaondoa ila msimuonee mtu. Nataka mkawe mitume kwa niaba ya Serikali,” alisema.
Magufuli alisema amewateua viongozi hao kwa kuwaamini na hatarajii itafika siku atajutia uteuzi wake na kubaini kuwa aliwateua kimakosa.
Makamu wa Rais
Kwa upande wake, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan aliwataka wakurugenzi hao kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa kuwa kuhudumia na kusimamia watumishi wa umma na wananchi; na si kuwa watawala.
“Kila mtu ajiulize kwa nini Tanzania kwenye watu takribani milioni 50, lakini ameteuliwa yeye. Someni alama za nyakati na muwatumikie vyema wananchi. Someni pia mazingira ya kazi, simamieni utendaji wenu kwa misingi ya sheria na katiba,” alisema Samia.
Waziri Mkuu
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema nafasi ya ukurugenzi katika halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji ni sawa na injini ya uwajibikaji, hivyo wanaoshika nafasi hizo wanatakiwa kuwa wachapakazi, waadilifu na wenye kujituma ili serikali na taifa kwa ujumla lifikie malengo yake.
“Nawataka mkifika muanze kwanza kuwafahamu vyema washirika wenu kama vile mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya, kamati ya ulinzi na usalama, sekretarieti ya mkoa, wakuu wa idara na watumishi. Zijueni vyema ofisi zenu tambueni maeneo yenu ya kazi,” alisema Majaliwa.
Aidha, alisema halmashauri pamoja na kuendeshwa kwa fedha za serikali pia zina vyanzo vyake vya ndani vya mapato na kuwataka viongozi hao kuwa mstari wa mbele katika kusimamia vyema vyanzo hivyo na ukusanyaji wa mapato yake.
Aliwataka kuwa mstari wa mbele kusimamia kikamilifu utekelezaji wa maagizo ya Rais likiwemo agizo lake la hivi karibuni la kuhakikisha kila mwanafunzi wa shule za msingi na sekondari ana dawati.
Ma-DC Pamoja na wakurugenzi hao kuapa kiapo cha uadilifu, pia wakuu wa wilaya watatu ambao ni Mkuu wa Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Nurdin Babu, Agnes Hokororo (Manyoni - Singida) na Miraji Mtaturu (Ikungi – Singida) walikula kiapo hicho.
Ma-DC hao hawakula kiapo cha uadilifu na wenzao hivi karibuni baada ya kubainika makosa katika uteuzi wa wateule wa awali wa nafasi za wilaya hizo. Hokororo alichukua nafasi ya aliyeteuliwa kuwa mkuu wa wilaya hiyo awali, Fatma Toufiq kutenguliwa kwa kuwa tayari ana wadhifa wa ubunge Viti Maalumu.
Babu na Mtaturu walichukua nafasi hizo baada ya wateule wa awali ambao ni Fikiri Avias Said na Emile Ntakamulenga, kutenguliwa uteuzi wao baada ya kuteuliwa kimakosa.
Kwa upande wake, Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Salome Kaganda aliwataka viongozi hao kuhakikisha wanazisoma na kuzielewa sheria zinazowaongoza ikiwemo Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Aidha, aliwataka kuhakikisha wanatunza maadili yao kama viongozi wa umma na kutambua kuwa wao na viongozi wa umma kwa saa 24 usiku na mchana hivyo wajiepushe na masuala yatakayowavunjia heshima na kuwaaibisha mbele ya jamii.
“Lakini pia nawahimiza mkumbuke kuwa nyie mtakuwa na siri nyingi za serikali haitopendeza kumkuta mbunge ana nyaraka zilizoandikwa siri za serikali kutoka eneo lako. Moja kwa moja utajibu,” alisema.
Jaji Kaganda alisema amebaini kuwa wateule wengi wa nafasi hizo za wakurugenzi ni vijana na kuwahimiza kuhakikisha hawaleweshwi na madaraka hayo na kujiingiza kwenye matendo ya anasa na kujivunjia heshima.
ConversionConversion EmoticonEmoticon