Mahakama yaamuru kesi ya Ester Bulaya iendelee

MAHAKAMA ya Rufaa imefuta uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza na kuamuru kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya (Chadema) iendelee kusikilizwa.
Uamuzi huo umetolewa baada ya Mahakama ya Rufaa kukubali hoja za rufaa ya kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyotupilia mbali hoja za kupinga matokeo hayo, ambazo ziliwasilishwa katika mahakama hiyo na wafuasi wanne wa aliyekuwa mgombea wa jimbo hilo, Steven Wassira (CCM).
Wafuasi hao; Magambo Masato, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na Escietik Malagila, walifungua kesi ya uchaguzi kupinga ushindi wa Bulaya katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, wakijitambulisha kuwa ni wapiga kura.
Awali, baada ya kesi hiyo kusikilizwa na Mahakama Kuu, Jaji Mohamed Gwae wa mahakama hiyo Kanda ya Mwanza, alitupilia mbali kesi hiyo baada ya kukubali pingamizi la wakili wa Bulaya, Tundu Lissu kuwa wafuasi hao hawakuwa na haki ya kisheria kufungua kesi hiyo.
Hata hivyo, walalamikaji hao hawakuridhika na uamuzi huo na kupitia kwa wakili wao Yassin Memba, walikata rufaa katika Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi huo, wakidai kuwa Kifungu cha 111 (1) (a) cha Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2010 kinawapa haki ya kufungua kesi hiyo.
Akisoma uamuzi wa mahakama ya rufani, ulioandikwa na jopo la majaji watano, Jaji Edward Rutahangwa, Ibrahim Juma, Stella Mugasha, Angela Kileo na Mussa Kipenka, Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Elizabeth Mkwizu alisema mahakama imekubali hoja za waleta rufaa kwa kuwa kifungu hicho cha sheria, kinawapa haki ya kufungua kesi kupinga matokeo hayo.
Kutokana na hilo, Mahakama ya Rufaa imefuta uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza na kuamuru kesi hiyo irudi ili hoja za walalamikaji zisikilizwe mbele ya jaji mwingine.
Previous
Next Post »