fahamu kuhusu ugomjwa wa surua


Hualigani msomaji wa mfululizo wa makala ya afya yako ambayo inakuletea kujifunza magonjwa mbalimbali visababishi pamoja na dalili,na jinsi gani ya kujikinga  na leo ninakuletea ugonjwa wa surua ambao nao umekua ni tishio hasa kwa watotot wadogo.

Surua ni mojawapo ya magonjwa ya kuambukiza yanayotisha kwa binadamu. Huu ni ugonjwa ulio na kiwango cha juu cha karibu asilimia 100 cha mashambulizi pindi mtu apatapo vimelea vya ugonjwa huu.


Pamoja na kuwepo chanjo ya ugonjwa huu, bado surua ni miongoni mwa magonjwa yanayosababisha vifo vingi vya watoto walio chini ya umri wa miaka 5 katika baadhi ya maeneo duniani hasa kwa nchi zinazoendelea.

Ugonjwa huu ambao ulitoweka katika baadhi ya nchi, umeanza kuonekana tena hivi karibuni miongoni mwa watu ambao hawakupata chanjo katika nchi za Uingereza na nyingine za Ulaya.


Nini husababisha surua


Surua huenezwa na aina ya virusi jamii ya paramyxovirus. Jamii hii ya virusi hupatikana katika mfumo wa njia ya hewa. Hukaa katika kamasi na majimaji yaliyopo katika mfumo wa hewa. Kwa sababu hii basi virusi hawa huenezwa kwa njia ya upumuaji.


Virusi hawa wanaweza kuishi hewani kwa muda wa hadi saa moja baada ya kutolewa kwa kupiga chafya au kukohoa au hata mazungumzo na mgonjwa. Hii ina maana kuwa, ili kuambukizwa surua, si lazima mtu akutane uso kwa uso na mgonjwa.
Baada ya kuingia ndani ya mfumo wa hewa virusi hushambulia seli za utando wa nje wa njia ya hewa (respiratory tract epithelium) na kuingia katika mzunguko wa wa limfu na kufika kwenye tezi zilizo karibu. Katika tezi huzaliana zaidi na kusambaa mwilini.


dalili za surua

[​IMG]
Dalili za awali za surua huanza kuonekana baada ya siku 8 ya kupata uambukizi. Mgonjwa huwa na mafua mepesi, homa, kukohoa na macho kuwa mekundu.


Baada ya siku 2-4 tangu kuanza kuonekana kwa dalili za awali, ukichunguza mdomo wa mtoto, na kama utamchunguza pembeni (ndani ya shavu) utaona vidonda vyeupe kwenye utando mwekundu wa ndani ya mdomo. Vidonda hivi huonekana kama chumvi iliyomwagwa kwenye zulia jekundu. Vidonda hivi huitwa Koplik spots. Hii ni dalili tosha ya kuthibitisha uwepo wa surua.


Lakini vilevile mgonjwa anaweza kuwa na vipele vidogo sana ambavyo inaweza kukuwia vigumu kutambua. Vipele hivi huweza kuonekana vizuri siku mbili baadaye. Kwa kawaida, vipele hivi huanzia usoni au nyuma ya sikio na kushuka chini kabla ya kutapakaa mwili mzima siku zinazofuata. Vipele huongezeka na kuwa vingi kadiri siku zinavyopita. Kawaida hali hii ya vipele inaweza kuchukua kati ya wiki 1-2. Vipele hupotea baada ya siku 7 na kuacha ngozi iliyobabuka. Hata hivyo, kukohoa kunaweza kuendelea zaidi ya siku 10.


Athari za Surua ni zipi?

Ingawa baadhi ya wagonjwa hupona katika kipindi cha siku 10 mpaka 14, baadhi hupata matatizo zaidi yanayoweza kuwa ya muda mrefu kama;

Maambukizi njia ya masikio (Otitis media)

 Maambukizi njia ya chini ya mfumo wa hewa kama vile;

 Uambukizi kwenye mirija ya hewa ya koo (bronchitis) maambukizi kwenye njia ya sauti (laryngitis) na croup. Surua inaweza kusababisha kuvimba katika sehemu ya sauti na kuathiri uwezo wa kutoa sauti lakini vilevile inaweza kusababisha uvimbe katika kuta za utando wa njia ya hewa.

Homa ya mapafu (pneumonia) ambayo ni sababu kuu inayosababisha vifo vinavyotokana na surua. Mgonjwa wa surua ni rahisi kupata homa ya mapafu kwa sababu kinga ya mwili wake huwa imepungua. Homa hii ya mapafu yaweza kusababishwa na aina nyingine ya virusi kama adenovirus, herpes simplex au bakteria kama Staphylococcus aureus, Streptococcus pneumonia, Haemophillus influenza, Klebsiella pneumonia. Lakini vilevile Kifua kikuu kinaweza kutokea kwa kusababishwa na upungufu huu wa kinga mwilini.

Surua pia inahusishwa na aina mbalimbali ya mashambulizi kwenye ubongo kama vile

Acute encephalitis ambayo hutokea wakati au ndani ya wiki chache baada ya maambukizi.

Progressive encephalitis ambayo hutokea kwa wagonjwa walio na upungufu wa kinga mwilini unaotokana na sababu yeyote ile ikiwemo wale anaopata tiba ya kemikali (Chemotherapy) au kwa sababu ya VVU. Hali hii hutokea miezi 6 baada ya maambukizi, na inaweza kusababisha mgonjwa kufa.

Subacute sclerosing panencephalitis (SSPE) ni nadra sana kutokea. Iwapo ikitokea, mara nyingi huwa ni mwaka mmoja wa mgonjwa kupona surua. Dalili mojawapo ya tatizo hili ni kupungukiwa kwa uwezo wa kufikiri, akili kuzorota na hatimaye mgonjwa kufariki dunia.

Surua inaweza kusababisha utapiamlo kwa sababu ya ukali wake hasa kwa watoto ambao hawapati lishe nzuri. Inahusishwa pia na kuharisha na kutapika na kusababisha upungufu wa maji mwilini.

Surua husababisha upungufu wa Vitamini A na kusababisha tatizo la kutoona vizuri ambalo hijulikana pia kama Keratitis. Kwa mtoto ambaye ana upungufu wa Vitamini A tatizo la macho huwa kubwa zaidi na kwa kitaalamu hujulikana kama Keratomalaciaambapo sehemu nyeupe ya jicho hutoboka.

Maambukizi katika misuli ya moyo (Myocarditis)

Upungufu wa chembe sahani kwenye damu (Thrombocytopenia)

Utambuzi wa surua

Utambuzi wa surua inajumuisha historia ya mgonjwa kuwa na homa kwa angalau siku 3 na kuwepo kwa mojawapo ya dalili za mwanzo za surua ambazo ni kukohoa, kuwa na mafua mepesi, macho kuwa mekundu na upele mwilini. Aidha ikithibitika mgonjwa ana Koplik spotsbaada ya uchunguzi ndani ya mdomo ni utambuzi tosha wa surua.


Vilevile vipimo vya kimaabara ni pamoja na uthibitisho chanya wa antibodi dhidi ya surua(measles IgM antibodies) na uwezekano wa kuwapata virus wa surua kutoka katika mfumo wa hewa, damu au mkojo wa mgonjwa (isolation of measles virus RNA) au kwa njia ya kuoteshwa maabara (culture).


Matibabu

Hakuna tiba maalum kwa ajili ya surua. Lengo kubwa la matibabu ya surua ni kuhakikisha mgonjwa anapata mapumziko, maji ya kutosha, oksijeni na faraja. Mgonjwa anaweza kupewa dawa za kutuliza homa kama vile paracetamol. Imeonekana kuwa matumizi ya dawa ya virusi wa surua (antivirus) hayana msaada wowote katika kutibu surua.


Aidha dawa kwa ajili ya kuzuia magonjwa yanayosababishwa na bakteria (Prophylactic antimicrobial therapy) isipokuwa tu iwapo itathibitika kuwepo kwa maambukizi ya bakteria. Inasisitizwa sana mgonjwa apatiwe Vitamini A. Vitamini A hupunguza hatari ya kifo na madhara ya surua.


Kwa vile ugonjwa wa surua unaenea kwa njia ya hewa ni vizuri mgonjwa akatengwa na watoto wengine. Muhimu ni kutafuta ushauri wa daktari haraka pale unapoona mtoto ana dalili za surua.


Kinga

Surua huzuiwa kwa urahisi kwa njia ya chanjo. Watoto ambao hawajapata chanjo ya surua wapo katika hatari kubwa sana ya kupata surua.


Kumbuka

Surua ni ugonjwa hatari. Unaweza kuua au kusababisha madhara ya muda mrefu lakini chanjo dhidi yake inazuia hatari hiyo. Kwa hiyo pale unapohisi mtoto wako ana dalili za surua mpeleke haraka hospitali ili kujithibitisha na kupata matibabu yanayofaa.


Previous
Next Post »