Ahlan wasahlan mpenzi
msomaji wa makala hii ya afya yako ambako tunaangazia zaidi magonjwa mbalimbali,
Na leo
tunazungumzia ugonjwa wa HEPATITIS wengi
tunafahamu kama homa ya ini.na Makala hii hukujia kila siku kwa hiyo ni kusihi usiache kufatilia
Hepatitis ni ugonjwa unaoshambulia ini unaosababishwa na virusi
vya Hepatitis B (HBV) ambapo kwa bahati mbaya licha ya kuwa hatari kuliko hata
Ukimwi kutokana na wepesi wa maambukizo yake, ugonjwa huo haufahamiki kwa
wengi. Taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaeleza kuwa, kirusi cha homa
ya ini kinaweza kuishi nje ya mwili wa binadamu kwa siku 7 na kwa wakati huu,
kirusi hiki kinaweza kusababisha maambukizi iwapo mtu hajapata chanjo ya
kuuzuia. Kwa sababu hiyo watu wengi wamekuwa wakiugua maradhi ya homa ya ini
bila kujua, hali ambayo hupelekea ini kuathirika taratibu.
Dakta Yuki Mark wa Hospitali ya Parktown North, Johanesburg, nchini Afrika Kusini anasema kuwa, homa ya ini aina ya B inaweza kuua kimyakimya bila kuonyesha dalili zozote. Dakta Yuri Mark anaeleza kwamba, huenda dalili zikaonekana waziwazi miaka mingi baada ya mtu kuambukizwa, na zinapoonekana, huenda tayari ini limenyauka au lina saratani na magonjwa hayo huua asilimia 25 ya watu walio na virusi vya HBV. Hepatitis A
Hepatitis A ni ugonjwa unaosababisha maambukizi katika ini ingawa si ya muda mrefu unaosababishwa na virusi vinavyoitwa Hepatitis A Virus (HAV). Kwa kawaida virusi vya ugonjwa huu hupatikana katika kinyesi cha mtu aliyeambukizwa na husambaa kwa kula chakula au maji yenye virusi vya ugonjwa huo. Inakadiriwa kuwa makumi ya mamilioni ya watu duniani huambukizwa ugonjwa huo kila mwaka duniani huku kipindi cha kuambukiza hadi kupona ugonjwa huo ni hadi miezi sita. Virusi vya HAV husababisha maambukizo makali na ya haraka katika ini lakini si ya muda mrefu wala ya kudumu, na karibu katika kesi zote za ugonjwa huu mwili huondoa virusi hivyo mwilini baada ya majuma au miezi michache. Maambukizo ya homa ya ini aina ya A ingawa si hatari lakini ni makubwa zaidi katika maeneo watu wasiyozingatia usafi, na kesi za ugonjwa huo hushuhudiwa kwa wingi hasa kwa watoto. Maambukizo ya ugonjwa huo hupungua katika sehemu ambazo watu wanazingatia matumizi ya maji safi na salama.
Dalili za Hepatit
Dalili za mwanzo za ugonjwa wa Hepatitis huweza kufanana na mafua na kwa kawaida hudumu kwa miezi isiyopungua miwili na baadhi ya watu huweza kuugua kwa muda wa miezi 6. Dalili zake ni uchovu, homa, kichefuchefu, kukosa hamu ya kula na homa ya nyongo ya manjano na kuonekana kiwango cha nyongo katika mkojo hali ambayo huufanya mkojo kuwa rangi nyeusi. Dalili nyingine ni kuharisha na kinyesi chenye rangi ya udongo.
Matibabu yake
Hakuna matibabu maalumu ya ugonjwa wa Hepatitis isipokuwa wale walioambukizwa hushauriwa kupumzika na kula lishe bora pamoja na kutokunywa pombe na kula vyakula vyenye mafuta mengi. Pia kujiepusha kula dawa ambazo haziwezi kuchujwa kwa urahisi na ini kama vile dawa ya kutuliza maumivu za acetaminophen, hadi daktari atakaposema kuwa ini limepona kabisa. Huenda mtu aliyeugua Hepatitis A asiambukizwe virusi hivyo tena katika maisha yake kwani mwili wake hujenga kinga lakini anaweza kuambukizwa aina nyingine ya maradhi ya virusi vinavyoshambulia ini. Chanjo inaweza kuzuia mtu asiambukizwe virusi vya HAV na tunaweza kujiepusha kuambukizwa ugonjwa huu kwa kudumisha usafi wa vyakula na mazingira yetu. Ugonjwa wa homa ya ini aina ya A kwa nadra sana huweza kusababisha ugonjwa wa muda mrefu wa ini.
Ili kujua kuwa mtu ana homa ya ini na wapo ameambukizwa ugonjwa
huo karibuni au muda mrefu uliopita anapaswa kufanyiwa vipimo kadhaa:
Kwanza ni kipimo cha HBsAg. hiki ni kipimo cha kuainisha iwapo
umeambukizwa virusi vya homa ya ini vya HBV na je, una uwezo wa kuwaambukiza
watu wengine au la? Kipimo hiki huchunguza aina ya antigeni ambayo ni sehemu ya
nje ya virusi na kupatikana kwake kwenye damu yako humaanisha kuwa una
maambukizo ya u Hepatitis B yaliyo hai na unaweza kuwaambukiza wengine kwa
urahisi.
Kipimo cha HBsAg kinapokuwa negative haina maana kuwa huna ugonjwa
huo kwa asilimia 100, bali pengine virusi vimelala, uliambukizwa zaidi ya miezi
6 iliyopita au chanjo yako bado ni imara.
Kipimo cha pili cha Hepatitis B ni Anti-HBs. Kipimo hiki ni cha
kuangalia iwapo mtu ana kinga ya virusi vinavyosababisha homa ya ini na iwapo
mwili umetengeneza antigeni ya kupambana na ugonjwa huo. Kuwa positive kipimo
hiki kunamaanisha hali mbili. Moja ni huenda ulipatiwa chanjo dhidi ya
Hepatitis B, na hali ya pili ni kwamba huenda uliambukizwa ugonjwa wa homa ya
ini humo nyuma. Katika hali zote mbili tulizozitaja iwapo kipimo cha Anti- HBs
ni positive inamaanisha kuwa huwezi kuwambukiza wengine ugonjwa huo na pia
virusi hivyo ingawa vipo mwilini mwako lakini vimelala na haviwezi kudhuru ini
lako kwa kuwa, mwili una kinga inayotokana na mfumo wako wa kulinda mwili.
Kipimo cha tatu cha ugonjwa wa Hepatitis B ni Anti-HBc, ambacho
huainisha iwapo uliwahi kuambukizwa ugonjwa huo huko nyuma au maambukizo ni ya
hivi karibuni. Kipimo hiki huangalia antibodi inayotokana na sehemu ya ndani ya
kirusi cha HBV inayopatikana kwa watu walioambukizwa ugonjwa huo. Iwapo kipimo
hiki ni positive inamaanisha kuwa, kuna uwezekano una maambukizo ya muda mrefu
ya homa ya ini yaliyo hai na unaweza kuwaambukiza wengine. Jawabu chanya la
kipimo hiki pia huweza kumaanisha kwamba, uliambukizwa zaidi ya miezi 6
iliyopita lakini haupo katika hali ya hatari.
Vipimo vingine vya nyongeza ni HBeAg na Anti-HBe ambavyo huonesha
kwa kiasi gani unaweza kuwaambukiza wengine ugonjwa huo na kiwango cha virusi
vya homa ya ini mwilini. Vipimo vyote hivyo tulivyovitaja iwapo vitakuwa
negative, basi inaamanisha huna ugonjwa wa Hepatitis B, na hivyo unapaswa
kupata chanjo dhidi ya ugonjwa huo. Kwa wale ambao hawana ugonjwa wa ini bali
walishawahi kupata chanjo dhidi ya ugonjwa huo, vipimo vyote tulivyotaja hapo
juu huwa negative isipokuwa kipimo cha Anti-HBs.
Kwa wale wanaopatikana na maambukizo ya ugonjwa huo, vipimo zaidi
hufanywa kama vile ultrasound ili kuonesha mabadiliko ya ini, kwani kama
tulivyosema virusi vya Hepatitis huathiri seli za ini. Baadhi ya wakati pia MRI
na CT scans hufanywa ili kuangalia uvimbe katika ini kwa watu ambao virusi vya
ugonjwa huo tayari vimewasababishia vidonda katika ini au kitaalamu liver
cirrhosis na pia kensa.
Kipimo kingine ni Alpha-foteprotein (AFP) kwa ajili ya kuangaliwa
kiwango cha protein aina ya AFP inayotengenezwa na seli za ini zilizo na
saratani. Kipimo hiki huonesha iwapo mgonjwa ana satarani ya ini au la.
Kipimo cha mwisho ni biopsy ya ini ambayo kwa ujumla huonesha
uzima wa ini. Kipimo hiki hufanywa ili kupata uhakika iwapo ini lina vidonda au
kensa.
Dawa yake:
Mtu ambaye ameambukizwa virusi vya Hepatiti anapaswa kwenda kituo cha afya au kumuona
daktari haraka. Kwa kawaida mwathirika hutakiwa kupata chanjo ya ugonjwa huo
ndani ya masaa 24 baada ya virusi kuingia mwilini ambayo huenda ikazuia
kujitokeza ugonjwa wa homa ya ini. Kwa wale ambao wamepatikana na maambukizo
lakini sio ya muda mrefu kwa kawaida hakuna matibabu yoyote wanayopewa bali
hupatiwa matibabu ya kupunguza dalili za ugonjwa huo wakati mwili ukipambana na
virusi vya HBV.
Watu wengi hupona kabisa ugonjwa huo baada ya miezi kadhaa bila
virusi kuharibu maini yao. Kwa kawaida hakuna matibabu ya homa ya ini ya muda
mfupi isipokuwa wagonjwa hushauriwa kupima damu mara kwa mara hadi pale virusi
vitakapoondoka mwilini. Lakini kwa wagonjwa wenye Hepatitis sugu ya muda mrefu,
wanapaswa kuonana na daktari maalumu anayehusika na magonjwa ya ini ili wapate
matibabu ya ugonjwa huo. Dawa zinazotolewa ili kutibu ugonjwa wa homa ya ini ni
dawa za kupambana na virusi kwa ajili ya kuzuia vijidudu vya Hepatitis
visiharibu ini na dawa hizo ni kama Entecavir, Interferon Alpha, Lamivudine,
Tenofovir n.k. Dawa hizo hutolewa ili kupunguza kasi ya madhara ya virusi
kwenye ini kwa kuzuia visizaliane zaidi na kusababisha vidonda au saratani ya
ini. Mgonjwa anapaswa kupata ushauri wa daktari kabla ya kutumia dawa hizo.
Lakini hata hivyo mgonjwa wa homa ya ini hata anayetumia dawa anaweza
kuwaambukiza wengine. Kwa sababu hiyo jambo muhimu kwa wagonjwa wenye maambukizo
ya Hepatitis ni kufanyiwa vipimo vya
damu mara kwa mara ili kujua matibabu yanavyokwenda na kujua iwapo kuna
mabadiliko yoyote katika ini. Jambo jingine muhimu ni mgonjwa kupata maelekezo
kutoka kwa wauguzi wa afya ili kuufahamu vyema ugonjwa wake na kuhakikisha
kwamba hasambazi na kuwaambukiza watu wengine ugonjwa huo.
Kinga ya Homa ya Ini:
ugonjwa wa homa ya ini una kinga inayoweza kuzuia maambukizo ya
virusi vya HBV. Ingawa kuna makundi maalumu ya watu wanaopaswa kupewa chanjo
dhidi ya ugonjwa wa Hepatitis lakini
katika nchi nyingi duniani chanjo hiyo hutolewa kwa watoto pindi wanapozaliwa.
Uchunguzi umeonesha kuwa, kuwapatia chanjo hii watoto pindi wanapozaliwa sio tu
kumepunguza hatari ya maambukizo kwa kiasi kikubwa bali pia kumepunguza kesi za
kensa ya ini. Watoto wote wanapaswa kupewa chanjo ya HBV wakiwa wachanga na
kumalizia dozi ya ugonjwa huo wanapokuwa na miezi 18. Pia watoto na vijana hadi
wa miaka 18 ambao hawakupatiwa chanjo hiyo walipokuwa wadogo wanapaswa pia
kupatiwa. Watu wengine wanaopaswa kupatiwa chanjo ya homa ya ini mbali ma wale
tuliowataja huko nyumba ni wanafamilia wanaoishi katika nyumba yenye mtu
aliyeambukizwa virusi vya HV. Hii inamaanisha kuwa, kwa wagonjwa wenye
Hepatitis , familia zao pia zinapaswa kupewa chanjo hiyo. Wengine ni wagonjwa
wa HIV, wagonjwa wa kisukari walio na umri chini ya miaka 60, wafungwa na
mahabusu, wanaofanyiwa dialysis, wenye magonjwa sugu ya ini, wanaosafiri kwenye
nchi zenye maambukizo makubwa ya homa ya ini na wanaofanya kazi za kuwahudumia
watu wasiojiweza.
ConversionConversion EmoticonEmoticon