AUWAWA KIKATILI MKOANI RUKWA

MWANAMKE mkazi wa Kijiji cha China Kata ya Kate, Nkasi, Rukwa, Telestina Silanda (45) ameuawa kwa kuchinjwa na mwili kucharangwa na watu wasiojulikana akiwa amelala nyumbani kwake usiku wa kuamkia jana.

Ndugu wa marehemu, Charles Silanda alidai tukio hilo lilitokea saa mbili usiku watu wasiojulikana waliovalia “kininja” walipovamia nyumba yake (shangazi) na kumshambulia kwa panga na kumchinja.

Alisema hadi wao wanajulishwa tukio hilo na kukimbilia eneo la tukio walikuta shangazi ameuawa na wauaji hao wametoweka katika eneo la tukio. Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Konrad Kauzeni alisema mwanamke huyo aliuawa kinyama, kwa kukatwa miguu yake yote miwili na kuitenganisha na mwili, kichwa na shingo.

Alisema mume wa mwanamke huyo alikuwa amekwenda porini kurina asali kwenye mizinga yake na aliporejea nyumbani alikuta mkewe kauawa kikatili na waliofanya tukio hilo hawajafahamika.

Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Said Mtanda ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo akisema ataenda kijiji hicho wananchi wapige kura za maoni ili kuwabaini wauaji hao.

Alisema ni jambo lisilokubalika watu kufanya uhalifu mkubwa kiasi hicho na wakaachwa, hivyo kura za maoni zitasaidia kuwanasa wauaji hao ili sheria ichukue mkondo wake. Aliwataka wakazi wa eneo hilo kwenda ofisini kwake kutoa taarifa za siri kwa wale wanaowafahamu.
Previous
Next Post »