Mwana wa mwanamapinduzi wa Cuba Fidel Castro, Fidel Ángel Castro Díaz-Balart, mwenye umri wa miaka 68 amejiua akiwa mji mkuu wa Havana, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali nchini Cuba vimetangaza.
Alipatikana akiwa amefariki Alhamisi asubuhi, na inadaiwa kwamba alikuwa anatatizwa na msongo wa mawazo.
Castro Díaz-Balart alifahamika sana kama "Fidelito" na alikuwa kifungua mimba wa rais huyo wa zamani wa Cuba aliyefariki dunia Novemba 2016.
Alifanya kazi kama mwanafizikia ya nyuklia, baada ya kupokea mafunzo katika uliokuwa Muungano wa Usovieti.
"Fidel Castro Diaz-Balart, aliyekuwa ametibiwa na kundi la madaktari kwa miezi kadha kutokana na msongo wa mawazo, alijitoa uhai asubuhi hii," gazeti rasmi la serikali ya Cuba, Granma liliripoti.
Runinga ya taifa imesema amekuwa akipokea matibabu miezi ya karibuni kama mgonjwa wa kutubiwa na kurudi nyumbani, baada yake kulazwa hospitalini kwa muda.
Kufikia wakati wa kifo chake, alikuwa mshauri wa kisayansi wa Baraza la Serikali ya Cuba na alihudumu kama makamu rais wa Chuo cha Sayansi cha Cuba.
Wasifu wake unaonesha aliandika vitabu kadha maishani mwake, na aliwakilisha taifa hilo katika hafla nyingi za kimataifa za kisomi kote duniani.
Tangazo kwenye televisheni limesema mazishi yake yatapangwa na familia yake, lakini maelezo zaidi hayakutolewa.
Babake, Fidel Castro, mwanamapinduzi aliyekuwa miongoni mwa viongozi waliotawala mataifa yao kwa muda mrefu, alifariki dunia akiwa na miaka 90 mwaka 2016.
ConversionConversion EmoticonEmoticon