Samia asisitiza miradi isimamiwe vyema


Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wanaosimamia mradi wa kuimarisha usimamizi wa maliasili na utalii - (REGROW) kusimamia vema mradi huo kwani fedha zinazotumika kuuendesha ni mkopo kutoka Benki ya Dunia ambao utalipwa na watanzania wote.
Akizungumza katika uzinduzi wa mradi huo utakaogharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 340 Makamu wa Rais amesema fedha hizo zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa kuendeleza utalii katika ukanda wa Kusini.
Utekelezaji wa mradi huo ni habari njema kwa wadau wa uhifadhi wa mazingira na utalii kwa Ukanda wa Kusini kutokana na vivutio vyake vingi kutofikika kwa urahisi kwa kuwa na miundombinu mibovu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza amesema kilio cha muda mrefu cha kuboreshwa miundo mbinu ya utalii kwa ukanda wa kusini kimesikika.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dokta Hamis Kigwangala amesema pamoja na kukuza utalii kuboresha kipato cha wananchi wanaozunguka hifadhi hizo, mradi huo pia utasaidia kukabiliana na vitendo vya ujangili. "Hapa anatuma salamu kwa majangili popote walipo", amesema.
Mkurugenzi mkazi wa Benki ya Dunia, Bella Bird amepongeza Serikali ya Tanzania kwa jitihada inazofanya katika uhifadhi wa raslimali kwa ajili ya kukuza uchumi hoja iliyoungwa mkono na Kaimu Chifu wa Kihehe Gerald Malangalila.
Previous
Next Post »