Kampeni kubwa imesambaa duniani wakati dunia leo inaadhimisha siku ya saratani duniani - #WorldCancerDay - kupiga vita saratani kwa kuongeza uhamasisho kuhusu umuhimu wa kutambua mapema na kuzuia kusambaa kwa saratani.
Shirika la afya duniani WHO linasema saratani ndio chanzo cha kifo cha mtu mmoja kati ya sita duniani, na hadi 50% ya aina zote za saratani zinaweza kuzuilika.
Lakini idadi ya visa vipya vya ugonjwa huo inatarajiwa kuongezeka kwa takriban asilimia sabiini katika miongo miwili ijayo.
Utumiaji tumbaku ndio hatari kuu ya chanzo cha kuugua saratani na ndio chanzo cha takriban 22% ya vifo jumla vinavyotokana na saratani.
Saratani ya matiti inaongezeka, hususan katika mataifa yanayoendelea, ambapo visa vingi hutambuliwa katika awamu ya mwisho wakati ugonjwa tayari umesambaa mwilini mwa muathiriwa.
Mambo kumi unayoweza kufanya kupunguza hatari ya kuugua saratani:
- Usivute sigara wala kutumia tumbaku ya aina yoyote
- Hakikisha nyumbani kwako hamna moshi
- Kula chakula chenye afya
- Kunyonyesha kunapunguza hatari kwa mama kuugua saratani
- Hakikisha watoto wako wanapata chanjo dhidi ya hepatatis B na HPV
- Epuka kuchomwa sana na miale ya jua, au tumia mafuta yanayo kukinga dhidi ya miale hiyo.
- Jishughulishe kuupa mwili mazoezi
- Punguza unywaji wa pombe
- Jitahidi kufanyiwa ukaguzi wa mapema kutambua uwepo wa saratani.
Nchini Kenya, ni ugonjwa wa pili unaochangia vifo vya watu baada ya magonjwa ya moyo.
Licha ya kuidhinishwa kwa baadhi ya malipo ya matibabu katika bima ya kitaifa ya afya nchini, bado tatizo lipo kutokana na kutowepo kwa taasisi za kutosha za umma zinazotoa huduma hizo - na kwa chache zilizopo, hazina vifaa vya kisawasawa.
Ni wachache wanaoweza kumudu gharama kubwa katika hospitali za kibinafsi.
Tanzania hali sio tofauti sana, wakati kunashuhudiwa uhaba wa vituo vya kutibu wagonjwa wa saratani - kuhudumia idadi jumla ya zaidi ya watu milioni 50 nchini .
Takwimu zinaonyesha kuwa saratani ya mfuko wa uzazi ni chanzo kikuu kwa wanawake wanaougua saratani Tanzania.
Kwa mujibu wa taasisi ya habari kuhusu kirusi cha HPV na saratani #ICO - tofauti na saratani nyingine, saratani ya mfuko wa uzazi inaweza kutambuliwa na kuzuiwa kabla ishike kasi na kusamabaa kwa ukubwa.
ConversionConversion EmoticonEmoticon