Wafanyabiashara wa tanzanite wabuni mbinu kukwepa kodi


WAFANYABIASHARA wa madini ya tanzanite na wamiliki wa migodi katika mikoa ya Arusha na Manyara, sasa wamebuni njia haramu ya kukwepa kulipa kodi ya serikali kwa kufanya biashara ya madini hayo, kwa njia za wizi.
Wafanyabiashara hao wameamua kuunda vikundi vya wachimbaji wadogo, maarufu kwa jina la ‘WanaApollo’ ili kuchimba kwa njia ya wizi katika Mgodi wa Kitalu C, unaomilikiwa na wawekezaji wazawa, Sky Associates Limited na Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (Stamico).
Tayari wafanyabiashara watano na WanaApollo 14, wamekamatwa kutokana na wizi huo na vyombo vya dola vinaendelea na uchunguzi wa wizi huo, unaoinyima serikali mapato ya madini hayo pekee yanayopatikana Tanzania.
Septemba mwaka jana, Rais John Magufuli aliliagiza Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kujenga ukuta wa kuzunguka vitalu vya kuanzia A hadi D vyenye madini ya tanzanite katika eneo la Mirerani, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara ili kudhibiti uchimbaji na biashara ya madini hayo.
Rais Magufuli alisema pamoja na kujenga ukuta huo haraka iwezekanavyo, soko la tanzanite litapaswa kuwa katika eneo hilo, tanzanite yote itapita kupitia lango moja na aliitaka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kushiriki katika ununuzi wa madini hayo.
Staili hiyo ya wizi iliyoshika kasi katika mgodi huo kwa muda sasa, inashirikisha vikundi 10 vya WanaApollo na baadhi ya wafanyakazi wa TanzaniteOne wakiwemo walinzi na viongozi, na hulipwa ujira mnono na matajiri wakubwa wa tanzanite.
Staili hiyo inawapa nafuu wafanyabiashara na wamiliki wa migodi, kupata madini kwa njia hiyo maarufu kwa jina ya ‘bomu’ bila ya kulipia hata senti tano serikalini katika uzalishaji huo.
Imethibitika kuwa baadhi ya wamiliki migodi ya tanzanite, wamesimamisha uchimbaji katika migodi yao ya kitalu B na D na kuendelea kufanya kazi hiyo, ambayo wamedai kuwa ina uhakika zaidi ya kupata madini na kusafirisha kwa njia ya panya kupitia Rwanda, baada ya njia ya Kenya kushtukiwa na kuwekwa ulinzi mkali.
Kugundulika kwa njama hizo, kumeelezwa na WanaApollo 14 waliokamatwa wakiwa ndani ya mgodi wa serikali na TanzaniteOne, Februari 3, saa 5:40 usiku, baada ya kukamatwa na walinzi wa kampuni hiyo.
Baada ya kukamatwa, wanadaiwa kuwa walieleza kwa kina kila kitu, ikiwamo kuutaja mtandao wa wafanyabiashara wakubwa wa tanzanite waliopo Arusha, Manyara na Kilimanjaro, wanaofadhili mpango huo wa kuvamia TanzaniteOne na kuchimba kwa wizi.
Baada ya taarifa hiyo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara liliwakamata wafanyabiashara wakubwa wa tanzanite na wamiliki wa migodi (majina tunayo), kwa uchunguzi zaidi. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Augustino Senga alithibitisha kukamatwa kwa wana Apollo hao na wafanyabiashara wakubwa wa tanzanite, akieleza kuwa uchunguzi wa kina unafanyika juu ya tuhuma zinazowakabili za kufadhili wachimbaji hao kuvamia usiku kwa njia ya panya.
“Tumewakamata wachimbaji wadogo wadogo na tayari wameshafikishwa mahakamani kujibu mashitaka na pia tuko katika msako wa kuwasaka wafanyabiashara wakubwa wa tanzanite wanaodaiwa kufadhili wizi huo na wengine tayari tumeshawatia mbaroni na tunaendelea na msako,” alisema Kamanda Senga kwa njia ya simu.
Aliongeza kuwa hawezi kutaja matajiri wanaoshikiliwa kwa mahojiano kwani wako katika uchunguzi zaidi wa kuwakamata wengine waliotajwa kuhusika na mtandao huo wa wizi haramu.
Wachimbaji waliokamatwa ni Ramadhani Marimi (45) mkazi wa Mirerani, Samwel Mathias (28) mkazi wa Arusha Esso, na wakazi wanne wa Mirerani Songambele, Julius Mollel (35), Calvin Michael (25), Samwel Okumu (46) na Godlove Kisaka (52) anayedaiwa kuwa kiongozi mkuu wa kundi hilo.
Pia Emmanuel Shaki (34) mkazi wa Kimashuku Kilimanjaro, Abdallah Mungwe (33) wa Mirerani Kazamoyo, Evarest Mollel (50) wa Arusha Balaa na Jonas Mollel (55), wa Ngulelo Arusha.
Kikundi hicho kilichokuwa na wana Apollo 14 kikiwa na zana zote za uchimbaji kilikuwa na wachimbaji wengine ambao ni Calvin Shayo (27) mkazi wa Mirerani Songambele, Tumaini Assey (29) mkazi wa Mererani Songambele, Julius Msaki (33) mkazi wa Shaghalai Arusha na Simon Evarest maarufu kwa jina la Mbongo mkazi wa Temeke jijini Dar es Salaam na pia ni mchimbaji wa kitalu D kinachomilikiwa na wachimbaji wadogo wadogo.
Akizungumza na gazeti hili, Kaimu Meneja wa Ulinzi wa Kampuni ya TanzaniteOne, Elisamehe Elias alisema wana Apollo hao walikamatwa katika mgodi wa JW uliopo ndani ya kitalu C, mali ya kampuni hiyo na serikali.
Elias alisema mgodi huo kwa sasa haufanyi kazi na walinzi wa zamu walishangaa waliposikia harufu ya petroli wakiwa lindoni usiku na kutoa taarifa kwa viongozi wa zamu na mtego uliwekwa ili kuwakamata wachimbaji hao.
Aliongeza kuwa baada ya kujisalimisha wana Apollo hao, viongozi wa TanzaniteOne, viongozi wa Wizara ya Madini na Shirika la Stamico, wote walijulishwa na kufika eneo la tukio na kuwahoji watuhumiwa hao na baadaye walipelekwa Kituo Kidogo cha Polisi Mirerani kwa mahojiano zaidi.
Naye Meneja wa Mgodi wa TanzaniteOne, Himid Didi alisema wao walishakamilisha kazi ikiwamo kuwakamata watuhumiwa hao na kuwafikisha katika vyombo vya dola ambao watafanya uchunguzi zaidi wa tukio hilo.
Previous
Next Post »