TANZANIA YA NYAKUA TUZO YA TECKNOLOJIA

SIKU chache baada ya Tanzania kunyakua tuzo za kimataifa za Uchumi Jumuishi na Utawala Bora, imepata tuzo nyingine mpya ya kimataifa iliyotokana na kuwa na teknolojia bora duniani.
Tuzo hiyo ambayo Tanzania imepata, inafahamika kama Tuzo za Kilele cha Serikali duniani (World Government Summit Awards) katika kundi la Tuzo ya Teknolojia bora inayoibuka Serikalini (Winner of the Best Government Emerging Technologies Award).
Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali cha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jana, ilisema tuzo hiyo ilitolewa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) Shehe Mansour Bin Zayed Al Nahyan.
Kwa upande wa Tanzania, aliyepokea tuzo hiyo kwa niaba ya Serikali ni Balozi wa Tanzania wa UAE, Mbarouk Nassor Mbarouk Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Tanzania ilikabidhiwa tuzo hiyo wakati wa kilele cha Mkutano wa Dunia wa Serikali (World Government Summit) uliohitimishwa jijini Dubai, Februari 13, mwaka huu.
Tuzo hiyo ilitokana na juhudi za Serikali ya Tanzania kupitia Taasisi ya Kilimo ya Mikocheni, kufanikiwa kulipatia ufumbuzi tatizo la maradhi ya zao la muhogo ujulikanao kitaalamu kama “Cassava Brown Creek Disease,” na “Cassava Mosaic Disease,” kwa kutumia chombo cha kisasa kinachoitwa “Portable DNA Sequencer”.
Maradhi hayo yanasumbua sana zao la muhogo, ambalo ni zao muhimu kwa Tanzania na nchi mbalimbali Afrika na duniani kwa ujumla. Kwa kutumia teknolojia hiyo mpya, wataalamu wanaweza kugundua magonjwa mbalimbali ya zao la muhogo yanayosababishwa na wadudu, virusi, bakteria na fangasi kwa muda wa siku mbili tu, kulinganisha na teknolojia ya zamani ambayo huchukua miezi kadhaa na ina gharama kubwa.
Zao la muhogo ni zao muhimu la chakula na biashara linalotegemewa, si tu na Tanzania, bali na nchi nyingine nyingi duniani. Inakadiriwa kuwa watu wapatao millioni 800 duniani, wanategemea zao la muhogo kwa chakula na biashara. Hivyo, teknolojia hiyo mpya itanufaisha nchi mbalimbali duniani katika kusaidia na kuendeleza zao hilo.
Nchi nyingine zilizopata tuzo hiyo ni India na Australia. Wakati huo huo, Watanzania wenye sifa wamehimizwa kuomba nafasi ya kazi iliyotangzwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya Mazingira (UNEP).
Maelezo kuhusu nafasi hiyo yanapatikana katika mawasiliano ya ttp://careers.un/bw/jobdetail.aspx?id=88749 na siku ya mwisho ya kuwasilisha maombi ni Februari 25, mwaka huu.
Previous
Next Post »